Auawa akimuokoa Mke aliyekuwa akipigwa na Mumewe

Mwanamume mmoja kutoka Gibarori, Kuria Mashariki katika kaunti ya Migori Kenya amepoteza maisha baada ya kuawa alipojaribu kuingilia vita vya jirani aliyekuwa akipigana na mke wake. 


Ripoti ya polisi inaonesha kuwa David Chacha mwenye umri wa miaka 32, alikuwa akizozana na mke wake Mary Chacha mwenye umri wa miaka 24, ambaye baadaye alitoroka na kukimbilia nyumbani kwa mama mkwe wake. Akiwa na hasira za mkizi, David alimfuata mkewe hadi nyumbani kwa mama yake ambapo alimpokeza kichapo zaidi.


Mama yake David, alipiga kamsa ambayo iliwaita majirani ambapo David alimpiga mmoja wa majirani hao na chuma kichwani na kusababisha jeraha kubwa kichwani.


"Polisi walitembelea eneo la tukio na kubaini kuwa David Chacha mwenye umri wa miaka 32, alikuwa na ugomvi wa kinyumbani na mkewe Mary Chacha mwenye umri wa miaka 24. 


Mkewe alitorokea kwa mamakwe ambapo David alimfuata na kumpiga zaidi," "Mama mkwe alipiga nduru ambapo jirani Ronald alifika kuwaokoa na kupigwa na chuma kichwani na David," ripoti ya polisi ilisoma kwa sehemu. 


Ronald alikimbizwa katika Hospitali ya Mother and Child ambapo alipewa rufaa hadi Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kehancha na baadaye katika Hospitali ya Migori Level 4 ambapo alithibitishwa kufariki alipowasili. Mshukiwa alikamatwa katika eneo la Motemorabu alikokuwa ametorokea na kulikuwa na taarifa kwamba alikuwa amekimbilia Tanzania.

“Baadaye mshukiwa alitorokea kusikojulikana lakini baadaye alifuatiliwa hadi Motemorabu alikokuwa amejificha,” ripoti ya polisi iliongeza. Mwili wa marehemu ulihamishiwa na kupelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Hospitali ya Kehancha ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti.

Chanzo: TUKO.co.ke 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo