Ajali ilivyokatisha uhai wa watu watatu wa familia moja

Tukio la ajali iliyokatisha uhai wa wanafamilia watatu wanatoka kwenye sherehe ya mahafali Kibaha mkoani Pwani, limeendeleza mfululizo wa ajali za kutisha na simazi kwa wanajamii.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa Novemba 26 mwaka huu, ambapo mama wa familia hiyo, Immaculata Byemerwa (49) pamoja na watoto wake wawili Jolister Byemerwa (17) aliyefanyiwa sherehe ya kuhitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari Gili ya Kibaha na Janeth Byemerwa  (20) mwanafunzi aliyekuwa anasoma mwaka wa tatu Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam walipoteza maisha baada ya ajali hiyo.

Hata hivyo, Albert Mrema aliyekuwepo kwenye gari hilo alinusurika katika ajali hiyo na sasa yupo chumba cha uangalizi katika Hospitali ya Mloganzila akipatiwa matibabu.

Chanzo cha ajali hiyo ya kusikitisha ilyotokea maeneo ya Kibamba jijini Dar es Salaam inaelezwa kuwa ni gari aina ya Prado Land Cruiser waliyokuwa wanasafiria kupoteza mwelekeo kwa kuacha njia na kuangukia kwenye bonde na kusababisha janga hilo.

Familia hiyo iliyokuwa na watoto saba inaingia kwenye majozi hayo mazito huku wakiwa na kumbukumbu ya mwaka mmoja umepita tangu wampoteze baba yao, Josephat Byemerwa aliyefariki Mei mwaka jana baada ya kuugua.

Patrick Mpochorwa mjomba na aliyekuwa wa kwanza kupokea simu ya ajali hiyo, amesema siku ya tukio waliondoka nyumbani kwao Tabata Kimanga saa nne asubuhi wakiwa watatu kwenye gari hiyo kwenda kwenye mahafali ya binti yao Julitha Byemerwa aliyehitimu kidato cha nne katika shule ya Gili Sekondari iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

“Sherehe ya mahafali yalifanyika salama na baada ya kuisha saa 12 jioni ndipo walipoanza safari ya kurejea nyumbani Dar es Salaam, ndani ya gari wakiwa wanne baada ya kuongezeka na binti yao aliyekuwa anafanyiwa mahafali siku hiyo.

“Wakiwa njiani kufika maeneo ya Kibamba walipata ajali iliyosababisha binti yao aliyefanyiwa sherehe ya mahafali hayo kufariki hapo hapo, huku wengine wakipata usaidizi kutoka kwa waliokuwa karibu kuwachukua na kuwapeleka zahanati iliyopo karibu na eneo la tukio,” amesimulia Mpochorwa.

Ameendelea kusema, baada ya kufikishwa kituoni hapo, kwa kuwa walikuwa wamepata ajali mbaya Albert aliruhusiwa kwenda Hospitali ya Mologanzila anakopatiwa.

Amefafanua alipigiwa majira ya saa moja usiku na hadi kufika eneo la tukio ilikuwa saa mbili usiku ndipo mashuhuda walimueleza waliopata ajali wamepelekwa Hospitali na baada ya kufika Hospitalini hapo alikuta misiba miwili.

Amesema Kwakuwa alikuta mili miwili ailianza kutafuta kujua wengine walikuwa wapi.

“Ndipo nilipoanza kuitafuta ile namba ya mtu aliyenipigia simu kwa mara ya kwanza ili anieleze iwapo anajua wengine walipo lakini muda mwingi simu yake ilionekana inatumika.

"Nikiwa Hospitali hapo nawaza ghafla ilikuja gari moja (Kirikuu) iliyokuwa imebeba mwili mmoja pamoja na ndugu yetu mwingine aliyenusurika katika ajali hiyo aliyepo kwa sasa chumba cha uangalizi Hospitali ya Mloganzila akipatiwa matibabu," amesema.

Mpochorwa amesema wanahisi mtarimbo wa kusukuma gari ulichomoka na kusababisha chombo hicho kupoteza welekeo na kuangukia kwenye bonde ambako ilionekana ilibinuka mara kadhaa.

Naye Prince Byemerwa, ambaye ni mtoto mkubwa wa familia hiyo amesema vikao vinaendelea na ndugu zake wanatarajiwa kuzikwa siku ya Alhamisi baada ya kufanyika ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania lilopo Tabata Magenge.

Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa kitengo cha usalama barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, William Mkonda azungumzie ajali hiyo alisema atafutwe Kamanda wa Polisi Kanda Maluumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro.

Hata hivyo, alipotofutwa Kamanda Muliro alisema "Nipo kweye kikao na kamati ya ulinzi nikimaliza nitakuwa katika nafasi nzuri ya kulifafanua tukio hilo.....," alisema Kamanda Muliro

Chanzo: Mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo