Lowassa: Msifanye Kosa Kuichagua CCM

Mgombea urais iliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa,  ametua katika Jimbo Singida Kaskazini la Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazoro Nyalandu, huku akiwatahadharisha wananchi wasipompigia kura za kuitosha kuiondoa CCM madarakani watakuwa wamejiangamiza.

Aidha, alimwelezea Nyalandu kuwa anamfahamu mbunge huyo kwa mbwembwe na nguvu ya fedha na kuhoji kama mgombea ubunge kupitia Chadema katika jimbo hilo, David Jumbe atamuweza.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Ilongero, Jimbo la Singida Kaskazini  jana ikiwa ni mfululizo wa ziara zake ya kuomba ridhaa kwa wananchi wamchague awe rais wa awamu ya tano, Lowassa alisema CCM itaondolewa madarakani kama wananchi wengi watajitokeza kupiga kura ya kuikataa.

“Watu wanataka mabadiliko ya maisha yao na sisi tumejitolea kuleta mabadiliko hayo,suala la kura ni muhimu sana mabadiliko yatakuja kwa kupiga kura tusipopata kura za kutosha tumeeangamia,” alisema.

Lowassa ambaye hadi sasa amefanya mikutano ya kampeni zaidi ya  32 katika majimbo ya mikoa 11 aliyotembelea, alisema CCM imeshindwa kuleta mabadiliko ya maendeleo na maisha ya wananchi yameendelea kuwa magumu.

“Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM Nilisema huwezi kuzuia gharika kwa mkono, sasa wameona gharika ya watu, tumekwenda Mpanda, Tabora, Iringa na leo (jana) hapa kwenu hivyo hivyo watu ni wengi,” alisema.

Mgombea huyo wa Ukawa aliwataka  wananchi wasikubali kura ziibwe na kutaka apatiwe kura si chini ya milioni 12 ili awe Rais.

Alisema serikali ya CCM imekuwa ikiahidi mambo mengi lakini haiyatekelezi na kwamba serikali atakayoiunda itakuwa ya vitendo kwa kutekeleza mambo yote.

Lowassa aliahidi akichaguliwa ataanzisha viwanda  vya alizeti na vitunguu ili viwe vinasafirishwa kwenda masoko ya nje.

 Kuhusu Nyalandu                    
Akimzungumzia Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Nyalandu, alisema anamfahamu kwa mbwembwe nyingi.
 
“Namfahamu Mbunge wenu wa sasa, namfahamu kwa mbwembwe zake sasa namulize Jumbe (mgombea Chadema) utamuweza maana kuna nguvu ya pesa na nguvu ya mtu,” alisema.

Hata hivyo, Jumbe alijibu kuwa tayari ameshamshinda Nyalandu.
 
Katika hatua nyingine wazee wa mila wa kabila la  kimasai na kinyatulu walimkabidhi Lowassa fimbo na mgolole ili aitumie kwa ajili kuwachapia wezi ili wasimzue kuingia Ikulu na kumtaka asiiache kila aendako.

Mgombea Ubunge CHADEMA
Naye mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Singida Kaskazini, David Jumbe, alimweleza Lowassa kuwa jimbo hilo linakabiliwa na kero za ubovu wa barabara, ukosefu wa soko la kuuzia mazao na hivyo wakulima kulanguliwa na wafanyabiashara.

“Mfano soko la vitunguu ikifika wakati wa mavuno wafanyabiashara kutoka Kenya wanakuja kwa wingi na kununua vitunguu na kwenda kuviuza nje kama bidhaa iliyozalishwa nchini mwao,” alisema.

Alisema kama akichaguliwa, askari wote wa mgambo watapewa majembe wakalime kwa sababu kazi ya kusimama kwenye mageti kwa ajili ya kutoza ushuru haitakuwapo na miti iliyopo katika mageti hayo itageuzwa kuwa kuni. 

Tundu Lissu
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema CCM haiwezi kuleta mabadiliko yeyote na hata ahadi ya Sh. milioni 50 kwa kila kijiji ni danganya toto.

“ Lowassa ametukanwa na tumemsema sana lakini ukweli wa Mungu hakufanya kosa lolote binafsi na hata wanaomtukana leo ni kwa sababu ameondoka CCM na siyo kwa sababu ya kashfa ya Richmond” alisema.

Laurence Masha
Naye aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha, aliwataka  wananchi waiogope CCM, akisema  imesababisha mateso makubwa kwao.

“Mtakayemuona ananunua shahada za kupigia kura katika eneo lenu, makamateni, mshughulikie na mtoweni katika eneo lenu,” alisema.

Mgeja
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema wanaotoka ndani ya CCM ni watu safi na waonang’ang’ania ni wachafu.

“Tunapofanya mabadiliko tujiamini, Ikulu siyo ya Mangula wala Nape, nchi nyingi za Kiafrika zimefanya mabadiliko kwa kuviangusha vyama tawala kwanini isiwezekane Tanzania,” alisema.

Jimbo la Iramba Magharibi
Akihutubia wananchi wa mjini Kiomboi katika  Jimbo la Iramba Magharibi, Lowassa aliahidi kuwa akichaguliwa ataanzisha benki ya bodaboda.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo