MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza imemhukumu kunyongwa hadi kufa Regina Alex baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua mtoto Janeth Samson mwenye umri wa mwaka mmoja kwa kumtumbukiza kisimani.
Mahakama hiyo imemtia hatiani kunyongwa hadi kufa mshtakiwa huyo baada ya kuridhishwa na ushahidi wa kimazingira pamoja na ushahidi wa mashahidi wanne na kielelezo kimoja vilivyotolewa mahakamani hapo.
Hukumu dhidi ya Regina Alex imetolewa na hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Cleofas Waane, ambapo amesema kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha sheria namba 167na 168 cha sheria ya adhabu.
Awali, mwendesha mashtaka wa Serikali, Monica Matwe aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 30, 2019 saa moja usiku katika kijiji cha Liyobahilika wilayani Bukombe mkoani Geita.
Mshatakiwa huyo anadaiwa kumtumbukiza kisimani mtoto wa jirani yake katika nyumba waliyokuwa wamepanga baada ya mzazi wa mtoto huyo Happiness Jonh kumuacha nje na kwenda bafuni kuoga.
.jpg)