Ni kundi la watu sita ambao walikuwa wakijihusisha na kazi ya omba omba wamenusirika kushushiwa kipigo na wananchi wa Mji wa Tarakea Kata ya Tarakea wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro baada ya kubainika kuwa watu hao ni matapeli ambao wamekuwa wakitumia kigezo kuwa wao wana ulemavu wa miguu.
Usiku wa kuamkia Oktoba 4,2022 katika Baa pamoja na nyumba ya kulala wageni iitwayo Nairobi Park iliyopo Tarakea Rombo kuliarifiwa kutokea vurugu ambazo zilielezwa kuwa ni ugomvi uliohusisha vijana wawili waliokuwa wakigombea mwanamke ambapo baada ya uongozi wa kijiji pamoja na wananchi kufika kwenye eneo hilo ndipo yakaibuka maneno ya kurushiana baina ya vijana hao wawili ambapo mmoja alisikika akimtuhumu mwenzake kuwa anaendesha biashara haramu ya kuwafanya watu kuomba wakijifanya wana ulemavu.
Inaelezwa kuwa baada ya wananchi waliokuwa hapo kusikia hivyo ndipo mmoja wa wale vijana alikimbia na baadaye uongozi wa kijiji ulifanya msako kwenye nyumba hiyo na kuwakuta watu hao wakiwemo watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wakiwa wamehifadhiwa na pia wanajishughulisha na kazi ya kuomba wakijifanya wana ulemevu huku ikibainika kuwa kijana aliyekimbia ndiye aliyekuwa amewaajiri kufanya kazi hiyo.