Serikali imesema ina mikakati ya kuhakikisha kila nyumba inakuwa na mtungi wa gesi ya kupikia na kuandaa mifumo mbalimbali kupitia uvumbuzi wa kibiashara ikiwemo kutumia teknolojia ya kupima gesi kidogo kidogo.
Hayo yamesemwa leo, Oktoba 21, 2022 na Waziri wa Nishati, January Makamba alipokuwa akihojiwa katika kituo cha televisheni cha Clouds kupitia kipindi cha Clouds 360.
Amesema utamaduni wa Watanzania ni kununua vitu kidogo kidogo hivyo wengi hawaoni unafuu wa gesi kwa kuwa inauzwa katika mitungi mikubwa.
“Kuwa na mtungi wa gesi kila nyumba inawezekana ni suala la kujasiliana maeneo ya vijijini wengi wanasema hawawezi kumudu, wakala yuko mbali siwezi kujaza. Ifike wakati mtu akiishiwa gesi kuna namna anaweza kuipata kwa haraka ukiangalia takwimu Tanzania tupo chini ya kilo 2 kwa matumizi ya mtu mmoja kwa mwaka wenzetu wapo kilo 46 lazima tuangalie tunafanya nini.
“Serikali tumechukua hiyo changamoto na tunaifanyia kazi, tunaona kama Je? Serikali iweke ruzuku, kodi iondolewe au ni vinginevyo,” amesema.
January amesema wengi wana kipato kidogo na matajiri na wenye kipato cha kati wanaomudu ni wachache, hivyo inabidi Serikali iangalia namna ya kulisaidia kundi hilo.
“Mitandao ya simu walifanikiwa baada ya kuweka vocha ndogondogo, ili nishati safi ya kupikia ishindane na mkaa itawezekana tukitumia teknolojia kuwezesha hata gesi iuzwe kwa bando, pale pana mita unaweka mpesa unafungua mita unaingiza gesi ya Sh100 unapika inaisha zipo vumbuzi ikawa moja ya majawabu inawezekana kuweka mitungi kila nyumba, kupitia uvumbuzi wa kibiashara,” amesema.