Watu watatu wamefariki dunia mkoani Geita, wakiwemo askari wawili wa Jeshi la Uhamiaji baada ya wao kupata taarifa za uwepo wa wahamiaji haramu kwenye moja ya nyumba katika Kijiji cha Mtakuja wilayani Mbogwe mkoani humo na ndipo ilipotokea sintofahamu na wananchi kuwashambulia.
Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi SACP David Misime, na kusema tukio hilo limtokea majira ya saa 8:00 usiku wa kuamkia Oktoba 26, 2022, na kusema hadi sasa jumla ya watu sita wanashikiliwa kutokana na mauaji hayo.
SACP Misime ameongeza kuwa, tayari tume ya uchunguzi imekwishatumwa kwenda katika Kijiji hicho kufanya uchunguzi wa mazingira yote ili hatua zichukuliwe kulingana na ushahidi utakaotolewa.
Waliouawa ni Mkaguzi wa Jeshi la Uhamiaji Salum Msongela Mpole, na Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Gilbert Edward, na mwananchi mmoja aitwaye Juma Bundala na kwamba katika tukio hilo askari mmoja alijeruhiwa.