Shule iliyombadilishia namba ya mtihani mwanafunzi yafungiwa

Serikali imeifungia Shule ya Awali na Msingi ya Chalinze Modern Islamic kuwa kituo cha Mitihani kutokana na udanganyifu uliofanyika katika Mtihani wa darasa la Saba uliofanyika Oktoba 5 na 6, 2022.


Hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyika uchunguzi kufuatia taarifa zilizotolewa na mwanafunzi Iptisam Suleiman Slim wa kituo cha Mtihani wa shule ya Awali na Msingi cha Chalinze Modern Islamic akieleza kwamba alibadilishiwa namba yake ya mtihani wakati akifanya mtihani wa somo la mwisho.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema uchunguzi uliofanywa na Kamati ya Mitihani ya Mkoa wa Pwani na ule wa wataalamu wa miandiko "forensic" uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini ufanano wa miandiko kwa watahiniwa 7 wa shule hiyo .

Waziri Mkenda amesema kwa kuwa kulikuwa na uzembe uliofanyika pamoja na kuifungia shule hiyo watumishi wa Serikali ambao walikuwa wasimamizi wa kituo hicho watachukuliwa hatua za kinidhamu huku akimuagiza mmiliki wa shule ya Awali na Msingi ya Chalinze Modern Islamic kuwafukuza kazi walimu wote waliohusika katika udanganyifu huo.

“Kwa kuwa shule hii ni ya binafsi tunaifungia kuwa kituo cha mitihani na haitaruhusiwa kufanyia tena mitihani, lakini pia mwenye shule hakikisha unawafukuza kazi mara moja walimu wote waliohusika na kama hilo halitafanyika nakuagiza Kamishna wa Elimu kufuta usajili wa shule hiyo na kuifunga mara moja,” amesema Waziri Mkenda.

Aidha kufuatia changamoto hiyo Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefanya marekebisho ya namba za Mtihani za watahiniwa husika ili kila mtahiniwa aweze kupata matokeo yake halali.

Kwa upande wake mzazi wa mwanafunzi Iptisam, Suleiman Said ameishukuru Serikali kwa kufanyia kazi changamoto hiyo aliyoipata mtoto wake wakati wa kufanya mitihani yake ya kuhitimu darasa la Saba. Pia amevishukuru Vyombo vya Habari kwa kutoa taarifa hiyo na kuweza kuwafikia walengwa na kuifanyia kazi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo