Picha za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Legazpi, nchini Ufilipino wakiwa wamevalia kofia za kuzuia udanganyifu walipokuwa wakifanya mitihani yao ya mwisho zimesambaa mitanadoni kote ulimwenguni.
Wanafunzi wote walifika kwenye jumba la mtihani wakiwa na kofia aina tofauti ambazo walitengeneza nyumbani kwao kwa kadibodi, masanduku ya mayai na vitu vingine. Hii ni kufuatia agizo la usimamizi wa shule.
Wanafunzi wengine walivalia miwani mirefu ili kuwazuia kutazama vijitabu vya majibu vya majirani wao au kuwauliza maswali wakati wa mtihani.
Picha hizi ziliwafanya walioziona kutoficha vicheko vyao kwenye mitandao za kijamii huku wengi wakionyesha kupuuza hatua hiyo na wengine kuunga mkono ubunifu uliotumika.
Mwalimu anayefahamika kama Mary Joy Mandane-Ortiz aliyebuni njia hii, akizungumza na kituo cha habari cha BBC, alisema kwamba amekuwa akitafuta njia mwafaka na itakayohakikisha kuna uadilifu na uaminifu katika darasa lake.
Profesa huyo alisema wazo hilo, ingawaje baadhi walipuuza lilikuwa lenye ufanisi mkubwa wa kupindukia.
Picha za wanafunzi hao wakiwa wamevalia kofia walizotengeneza kutumia ubunifu wa hali ya juu ziliwapendeza wengi.
Pia inasemekana walimu wakuu wa shule na vyuo vikuu katika maeneo mengine ya nchi hiyo wanalenga kuiga mbinu hiyo kuzuia udanganyifu wa mitihani shuleni.
Prof Mandane Ortiz alisema wanafunzi wake walifanya vyema zaidi mwaka huu, baada ya kuanzisha mbinu hiyo na kuwekwa kwa masharti magumu ya mitihani kwani iliwafanya wanafunzi kusoma kwa bidii zaidi.
Wengi wao walimaliza majaribio yao mapema, aliongeza - na hakuna mtu aliyekamatwa akidanganya mwaka huu.
Chanzo - BBC