VISA vya ukatili wa kijinsia vinazidi kushika kasi katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, safari hii mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 15 anadaiwa kunajisiwa kwa ahadi ya kupewa Sh. 2,000, kununuliwa simu janja na begi la shule.
Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) kwa sasa amekatisha masomo yake baada ya kupata ugonjwa wa zinaa uliotokana na kufanyiwa ukatili huo na mtu anayedaiwa kuwa rafiki mkubwa wa baba yake mzazi.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo, mtuhumiwa anayetajwa kufanya tukio hilo, Alfred Njau (38) alikamatwa Oktoba 8 mwaka huu na baadaye aliachiwa kwa dhamana.
“Ni kweli tulimkamata na kumshikilia Njau katika Kituo cha Polisi Majengo kutokana na tuhuma za unajisi, lakini baadaye tulimwachia kwa dhamana. Upelelezi wa tukio hili utakapokamilika tutamfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo,” alisema.
Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo ambaye ni Mkazi wa Kitongoji cha Kikowonyi, Kijiji cha Mwasi Kusini, Wilaya ya Moshi, alianza kunajisiwa na mtuhumiwa huyo Januari mwaka huu.
Hata hivyo, mwanafunzi huyo anadai kuwa hakutoa taarifa za vitendo hivyo kutokana na vitisho alivyokuwa akipewa na mtuhumiwa kwamba akitoa siri hiyo, atamuua.
Akizungumzia tukio hilo, Helena Temba ambaye ni bibi anayeishi na mwanafunzi huyo, alisema aligundua mjukuu wake kubadilisha mwendo wa kutembea na kila alipomuuliza alikuwa akimwambia tumbo linamuuna.
"Mjukuu alikuwa hasemi tatizo linalomsibu hadi juzi alivyoamua kueleza ukweli, kwamba alikuwa akifanyiwa ukatili na jirani yangu, ambaye alikuwa rafiki wa mwanangu.
"Sasa baada ya kueleza hilo tatizo ilibidi tumpeleke hospitalini na alipofanyiwa uchunguzi wa kitabibu alikutwa ameingiliwa sehemu za siri na ameambukizwa magonjwa ya zinaa," alisimulia.
Alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kikowonyi, Magdalena Maro alikiri kuwa taarifa hizo ni kweli.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwasi Kusini, Omary Sinari adai kuwa pamoja na mtuhumiwa kukamatwa, amerejea mtaani na anaendelea na kujigamba baada ya kuachiwa kwa dhamana.
Chanzo: Nipashe