Jela miaka 30 kwa kumnajisi mwanawe wa kumzaa

ELIHURUMA Mwandri (46), Mkazi wa Kijiji cha Lomakaa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, amehukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya hiyo kwa kosa la kumnajisi mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka saba.

Jana wakati Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Elibahati Petro, akisoma hukumu hiyo, alisema amelazimika kumpa adhabu hiyo mshtakiwa Elihuruma baada ya kuridhika na namna upande wa mashtaka ulivyofanikiwa kuijenga kesi hiyo ambayo ushahidi wake hauachi shaka yoyote.

“Nimepitia mwenendo mzima wa kesi hii na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, yaani upande wa mashtaka na upande wa utetezi nimejiridhisha pasipo shaka kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo, hivyo kwa mujibu wa sheria anahukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 gerezani,” alisema.

Wakati anasoma hukumu hiyo, Hakimu Elibahati alisema upande wa mashtaka katika kesi hiyo ulikuwa na mashahidi watano, akiwamo daktari aliyefanya uchunguzi wa kitabibu, mwanaharakati, mama mzazi na mwathirika mwenyewe.

Kwa mujibu wa Hakimu huyo, mshtakiwa alikuwa akiishi na mwanaye huyo (jina limehifadhiwa) huku akiwa ametengana na mzazi mwenzake.

Alisema, malezi hayo ya upande mmoja yalimrahisishia mshtakiwa kufanya ukatili huo ambao ni kinyume cha Kifungu cha 130 (1) (2) (e) na kifungu 131 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2019.

Baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani, mahakama hiyo ilimpa nafasi ya kujitetea ambapo mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu anaishi na mama yake mzazi ambaye ni kikongwe anayemtegemea kumtafutia chakula, vilevile yeye mwenyewe ni mgonjwa.

Katika maelezo ya kosa, ilidaiwa mahakamani huko kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 16 mwaka huu katika Kijiji cha Lomakaa, Kata ya Kirua kwa kumnajisi mtoto huyo, huku akitambua kwamba kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Mwendesha mashitaka wa Serikali, David Chishimba, alidai mahakamani huko kwamba mtoto huyo akiwa Shule ya Msingi Lomakaa, alifichua ukatili huo wakati mwalimu wake akiwafundisha kuhusu madhara ya ukatili kwa watoto na namna ya kujikinga,

Mtoto huyo alimfuata mwalimu wake (jina limehifadhiwa) na kumweleza kuwa baba yake amekuwa akimfanyia ukatili kwa kumnajisi.

Kutokana na maelezo ya mtoto huyo, mwalimu wake alichukua jukumu la kutoa taarifa kwa mmoja wa wanaharakati na kisha mwanaharakati huyo kutoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi Sanya Juu ambako polisi walimsaka na kufanikiwa kumkamata mshtakiwa.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka huyo alisema, kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo katika jamii chisimba aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshitakiwa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo