Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amemtaka mganga mkuu wa Halmashauri ya Njombe Dkt. Suke Magembe kumuondoa kwa haraka daktari wa zahanati ya kijiji cha Igombola Samweli Tupa kilichopo katika kata ya Lupembe wilayani humo kwa kile kinachodaiwa kuwa na utovu wa nidhamu awapo kazini.
Uamuzi huo umekuja mara baada ya mkuu huyo wa wilaya kuwasili katika kata hiyo kukagua miradi ya maendeleo na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi hao uliolenga kusikiliza kero mbalimbali ambapo wananchi hao wakaibua kero hiyo na kumtaka mkuu huyo wa wilaya kuondoka na daktari huyo.
“Maelekezo yangu,kama mtumishi huyu ana barua leo uondoke naye ili isiendelee kuwa kero, lakini mtu kama huyu ambaye ana tabia mbovu na kukiuka maadili ya kazi kumuhamisha sio adhabu sasa ili tusimuonee mtu afunguliwe mashtaka kwa mujibu wa sheria za utumishi ili kama habadiliki atupishe aachie wengine wanyenyekevu kwa sababu tutampeleka tena sehemu nyingine wananchi tena wanamkataa."
Awali wananchi wa kijiji hicho walidai kuwa mganga huyo amekuwa mlevi pamoja na kushindwa kutibu wagonjwa mpaka watoe fedha za matibabu wakiwemo wazee kitu ambacho kinaweza kusababisha vifo kwa wagonjwa hivyo hali hiyo imejenga hofu kwa wananchi hao.
Kwa upande wake mganga Mkuu wa halmashauri hiyo amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kudai kuwa tayari wamekwisha chukua hatua za kumuondoa mtumishi huyo na kumrudisha makao makuu.