MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika chaguzi zote ni wa lazima kwa lengo la kuendelea kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Dk. Shein ambaye pia, ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyasema hayo leo katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Uguja uliopo Mahonda, Wilaya ya Kaskazini A, wakati alipozungumza na Mabalozi wa Wilaya ya Kaskazini A.
Alisisitiza kuwa katika uchaguzi CCM ni lazima ishinde kwa kutumia demokrasi, hoja za kisiasa pamoja na maandalizi ya ushindi na kusisitiza kuwa ushindi wa CCM una umuhimu katika kuyadumisha na kuyalinda Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwaeleza Mabalozi hao kuwa ushindi kwa CCM ni kuendelea kuulinda na kuutunza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Kaume na Marehemu Julius Kambarage Nyerere
Alisema kuwa Muungano huo ni wa kidugu na wa watu wenye asili moja walioungana kimaisha na kuwa wamoja na hata kuweza kuviunganisha vyama vyao vya TANU na ASP na hatimae kupatikana kwa CCM.
Alieleza kuwa wapo waliojaribu kutaka kuuvunja Muungano huo kwa kufanya vituko mbali mbali lakini wameshindwa na hatimae Muungano umeendelea kudumu hadi hivi leo na kusisitiza kuwa hakuna mtu hata mmoja atakaeweza kuuvunja Muungano huo.
Alieleza jinsi Serikali inavyopambana na rushwa na kusema kuwa wapo wanaochukua na kupokea rushwa na wapo walioiba fedha za Serikali na tayari wamechukuliwa hatua na wapo wanaoshitakiwa ambapo pia watatakiwa kuzilipa fedha hizo na hatimae kuchukuliwa hatua pale itakapobainika kufanya kosa hilo.
Aidha, Dk. Shein alisikitishwa na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto na kueleza kuwa wanaofanya vitendo hivyo wanaiondoshea Zanzibar heshima yake kwani ilikuwa ikitajika kwa maadili mema pamoja na elimu katika ukanda wote wa Afrika Mashariki.
Pia, Rais Dk. Shein aliwaeleza Mabalozi hao juhudi za Serikali katika kuimarisha miradi ya maendeleo katika Mkoa huo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mkwajuni-Kijini km 7.6, pia, Serikali inafanya jitihada ya kuibadilisha Matemwe.
Pamoja na ujenzi wa barabara ya Mkwajuni-Mbuyumaji yenye urefu wa km 22, Pale- Kiongele km 4.6 na Barabara ya Bububu hadi Mkokotoni kupitia Mahonda Kinyasini, Chaani hadi Mkokotoni ambayo itakuwa ya kisasa ambapo mjenzi yupo kwenye eneo la kazi hivi sasa na tayari fidia imeshatolewa. “Kaskazini itafumbuka tutajenga mji wa kisasa Mkokotoni na tushaamua”, alisisitiza Dk. Shein.
