Kituo hicho cha afya ambacho kilianzishwa mwaka 1978 kinachotegemewa na wakazi wa Tarafa ya Grumeti, kimepata Tsh400 milioni kutoka serikalini kwa ajili ya kuboresha miundombinu.
Hata hivyo, bado kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchafu wa maeneo.
Malima alifanya ziara juzi saa mbili usiku na kukuta vibatari vikitumiwa chooni huku kukiwa hakuna taa.
Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa mkoa alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri kuhakikisha taa zinawekwa.
“Naagiza wewe uweke umeme, mapato ya halmashauri mnayafanyia nini wakati hawa wananchi wanapata shida, nipate taarifa ya utekelezaji,” aliagiza Malima.
Awali, Dina Joseph mkazi wa Natta aliyekuwa anahudumia mgonjwa alisema kwa zaidi ya siku mbili walikuwa wakitumia tochi za simu na vibatari.
“Chooni tunaenda gizani, kwa ujumla mazingira haya hayafai, tunaomba Serikali ichukue hatua maana huu ni kama udhalilishaji wa wagonjwa,” alisema Dina.
Huduma mbovu
Malima alisema wananchi wanapata huduma mbovu kwa sababu ya uzembe wa watu wachache na kwamba, Serikali haiwezi kukubaliana na watu wa namna hiyo.
“Akina mama wanajifungua kwa kutumia tochi na vibatari wakati jengo hili lina umeme, kuweka taa hapa mnashindwa, huu ni uzembe mkubwa,” alisema.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Selestine Simango alisema kulijitokeza hitilafu ya umeme katika eneo hilo na kwa sasa wanaendelea kufanya matengenezo.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri, Juma Hamsini alisema watafanya marekebisho ili umeme upatikane haraka.
Chanzo:swahilihub
