Mikoa 14 yaanza majaribio ya Kinga ya UKIMWI

Dar es Salaam. Serikali imesema mikoa 14 inashiriki majaribio ya dawa kinga mpya inayozuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kupitia makundi maalumu.
Pia, imesema watu wanaohusishwa na utafiti wa dawa hiyo ijulikanayo kama Pre-Exposure Prophylaxis maarufu PrEP, ni walio katika vihatarishi vya kuambukizwa VVU, huku ikikanusha kuwapo kwa dawa inayotibu maradhi hayo.
Dawa kinga hiyo ina uwezo wa kuzuia maambukizi ya VVU ikiwa mtumiaji atameza kila siku kwa muda wa siku saba kabla hajashiriki tendo la ngono na ataendelea kuimeza kwa kipindi chote atakachokuwa katika hatari ya kuambukizwa.
Hata hivyo, Serikali haijataja mikoa inayohusika na majaribio hayo.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa mpango wa nne wa VVU na Ukimwi katika sekta ya afya (HSHSP IV 2017-2022) na maadhimisho ya miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema taarifa kwamba nchi inazindua tiba dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi si sahihi kwa kuwa Tanzania bado haijapata tiba hiyo.
“Tumezindua dawa kinga, kuna dawa ambayo tunataka tuielekeze katika makundi ambayo tunayaona yapo kwenye hatari ya kuambukizwa VVU, watapatiwa kwa lengo la kuwakinga wasipate, ila si suluhisho na tuseme vilevile kwamba hatujapata tiba ya virusi vya Ukimwi na utaratibu huu wa dawa kinga ndiyo unaanza majaribio sasa,” alisema.
Dawa mpya zenye uwezo wa kukinga maambukizi dhidi ya VVU kwa asilimia 99 zilizoanza kutumika katika baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika, zinakuja wakati ukanda huo ukiongoza duniani kwa kuwa na asilimia 50 ya waathirika.
Utafiti uliofanywa na mwanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha London, Dk Sheena McCormack umeonyesha PrEP inazuia maambukizi ya VVU kwa kuua virusi baada ya kufanyiwa majaribio kwa kundi la wapenzi wa jinsia moja, ambao wamo katika hatari zaidi ya maambukizi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetambua kwamba dawa hiyo ya vidonge (tembe) inaweza kupunguza maambukizi kwa kiwango kikubwa.
Wakati huohuo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameagiza nusu ya vituo 3,400 vinavyotoa huduma ya kupima VVU kwa wajawazito vianze kutumika kupima na kuhudumia watu wanaoishi na VVU. Hata hivyo, alisema hajaridhishwa na kasi ya kudhibiti maambukizi.
“Tanzania imekuwa ikiridhia mapendekezo na malengo kutoka Shirika la Afya Duniani na lile la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (Unaids), lengo mojawapo ambalo nchi yetu iliridhia mwaka 2016 kutoka shirika hilo kuhusu kufikia 90 tatu ambazo ni kufikia asimilia 90 ya wanaoishi na VVU kujua hali zao, asilimia 90 watakaopimwa na kugundulika kuwa na maambukizi kusajiliwa kwenye mpango wa tiba na matunzo na asilimia 90 ya walioko kwenye tiba na matunzo kuwa na kiwango cha chini cha VVU, yote hayo ifikapo mwaka 2020.
Afrika Kusini, Botswana na Zimbabwe zimeanza kutoa dawa hiyo kwa makundi maalumu yaliyo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU.
Mwanaharakati wa kupambana na Ukimwi kutoka shirika la Avac la Marekani mwenye makazi jijini Gaborone, Botswana, Kennedy Mupeli alisema PrEP haizuii kupata maambukizo ya magonjwa ya ngono.
Tofauti ya PrEP, PEP na ARV
PrEP ni kwa ajili ya mtu ambaye hajaambukizwa VVU ili kujikinga na maambukizo.
ARV ni kwa ajili ya mtu ambaye tayari ameambukizwa VVU na anaitumia ili aweze kulinda kinga zake za mwili zisidhoofishwe na virusi.
PEP hutumika kumkinga mtu dhidi ya VVU ndani ya saa 72 baada ya kuhisi kuambukizwa kutokana na vitendo kama vile kubakwa.
Watu ambao ni hawajaambukizwa VVU walio katika hatari kama wapenzi wa jinsi moja na makahaba wamekuwa wanakingwa kwa kupewa dozi ya kila siku ya Truvada (mchanganyiko wa Emtricitabine na Tenofovir) ili kuwakinga dhidi ya maambukizo.

Credits: Mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo