Ma DC, wakurugenzi wasiosimamia usafi kukiona

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameziagiza Halmashauri zote na mamlaka nyingine zinazomiliki masoko zitenge fedha kwa ajili ya usafi wa maeneo hayo na maeneo mengine vikiwemo vituo vya mabasi kwa kuwa huo ni wajibu wao.
Ameagiza wakuu wa Wilaya, wakurugenzi na maofisa afya wa Halmashauri za wilaya wahakikishe maeneo yote ya kutolea huduma yakiwemo masoko yanaimarishwa miundombinu na usafi wote kwa ujumla wake na watapimwa kwenye jambo hilo na hatua zitachukuliwa kwa watakaozembea kuratibu hilo.
Ametoa agizo hilo bungeni wakati anajibu swali na Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni kwenye kipindi cha maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu.
“Si tu masoko, maeneo yote yanayohitaji kufanyiwa usafi ndani ya Halmashauri” amesema Waziri Waziri Mkuu.
Amesema, takribani halmashauri zote zinamiliki masoko na ndizo zinazotoza kodi na ushuru kwenye masoko hayo yakiwa ni mapato ya ndani na matumizi ya fedha hizo hupangwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri husika.
“Ni wajibu wa kila Halshauri kupitia Baraza la Madiwani kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za usafi kwenye maeneo yao, na tunapozungumzia usafi hatuzungumzii kufagia na kuzoa taka tu ni pamoja na kuimarisha miundombinu ili iwe rafiki kwa ajili ya kuendesha shughuli za biashara kwenye maeneo hayo na maeneo mengine…” amesema na kuyataja maeneo mengine kuwa ni pamoja na vituo vya mabasi na hospitali.
Majaliwa amesema, Rais John Magufuli alizindua kampeni ya usafi hivyo inatakiwa maeneo yote yawe safi hasa pia kwa kutekeleza agizo la kufanya usafi kila Jumamosi asubuhi.
“Kwa hiyo Halmashauri zinawajibika kusimamia, na viongozi wote wanajibika kusimamia ili nchi iweze kuwa safi na maeneo yake yote yakiwemo maeneo ya kutolea huduma likiwemo na eneo la soko” amesema.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo