BWAWA la Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, limejaa maji kupita uwezo wake na kutapika hivyo kuhatarisha maisha ya wakazi wanaoishi jirani.
Maji kwa sasa katika bwawa hilo yamefikia mita za ujazo 689.1 juu ya usawa wa bahari, kiwango ambacho ni cha juu na hutokea kila baada ya miaka 10.
Akizungumza na wanahabari juzi, msimamizi wa bwawa hilo kutoka Bonde la Pangani, Vendelin Basso alisema Mei 7 maji katika bwawa hilo yalifikia mita za ujazo 689.1 juu ya usawa wa bahari.
Basso alisema kujaa kwa bwawa hilo ni habari njema lakini wananchi wanaoishi jirani na Mto Pangani wanatakiwa kuchukua tahadhari, kwa kuwa iwapo mvua zitaendelea wanaweza kupata madhara makubwa.
Alisema kiwango cha maji kinachoingia katika bwawa hilo ni wastani wa mita za ujazo 280 na ‘hutapikwa’ yote kupitia mto Pangani.
“Tayari tumetoa taarifa kata zilizoko jirani na mto Pangani ambazo ni za Ngorika, Ngage, Loiborsoit kwa Wilaya ya Simanjiro; Kirya wilayani Mwanga na Ruvu na Mabilioni zilizopo wilayani Same ili wananchi wachukue tahadhari,” alisema Basso.
Kuhusu Mto Pangani, Basso alisema kwa sasa kina chake kimeathiriwa na magugu maji hali ambayo husababisha maji yanayotapikwa katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na kuingia kwenye mto huo kufurika na kusambaa kwa wananchi.
Naye meneja wa kituo cha kufua umeme cha Nyumba ya Mungu, Clarence Mavunda alisema uzalishaji umeme umeongezeka kutoka megawati 2.5 hadi nne.
“Hali ya maji kwa sasa inatia matumaini kwa kuwa awali hali ya maji ilikuwa mbaya na kutulazimu kutumia mashine moja,” alisema.
Tukio la kujaa kwa bwawa na kusababisha kutapika limekuwa likitokea kila baada ya miaka kumi, lilitokea mwaka 1988, 1998 wakati wa mvua za El Nino na kujirudia mwaka 2008.