Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa anahutubia leo (April 3, 2018) Jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa mradi wa kuzalisha umeme Kinyerezi 2, ambao unatarajiwa kuingiza megawatts 240 katika gridi ya Taifa.
"Sasa niwaombe Mawaziri, Makatibu wakuu, Watendaji, wenye viti wa bodi msiogope kuwasiliana nyinyi kwa nyinyi hakuna sababu ya miradi mikubwa kama hii kuonekana inakwama kwasababu ya kukosa tu kibali cha TANROADS au kushindwa kupata kibali cha maji, kibali cha ardhi. Mimi mambo haya huwa nikiyasikia yananiudhi kweli labda nitumie lugha ya mjini mnaweza mkanielewa yananiboa kweli kweli", amesema Dkt. Magufuli.
Pamoja na hayo, Dkt. Magufuli ameendelea kwa kusema "nyinyi wote ni watanzania, mnafanya kazi wote chini serikali ya awamu ya tano mshirikiane ili kusudi tusije kuingiza serikali katika gharama nyingine kubwa. Huu ni wito wangu nafikiri mwenye kusikia na asikie na wakutenda mkaanze kutenda".
Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amesema serikali kuhamia mkoani Dodoma haimaanishi kwamba wataweza kusahau dhamira yao ya kulifanya Jiji la Dar es Salaam liwe la Kisasa kama walivyoahidi hapo awali.
