Mtanzania auawa nchini Afrika Kusini

Mtanzania aitwaye Baraka Nafari amefariki dunia kwa kugongwa na gari na watu wasiojulikana akitokea katika matembezi.
Baraka ambaye alikuwa akisoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Johannesburg (UJ), Afrika Kusini aligongwa na gari alipokuwa akitokea matembezini usiku.
Akizungumza na MCL Digital leo Machi 2, 2018, Uwezo Edward ambaye ni binamu wa Baraka anayeishi Afrika Kusini amesema hana uhakika iwapo ndugu yake alikuwa na adui au ugomvi na mtu, lakini mazingira ya kifo chake yana utata, pia wanatagema kuuaga mwili wa kijana huyo siku ya Jumanne ijayo nchini humo kabla ya kuanza safari ya kuuleta mwili nchini.
“Alhamisi ya wiki ijayo tutausafirisha mwili wa mpendwa wetu kuelekea mkoani Kigoma kwa ajili ya kuupumzisha kwenye makazi ya milele,” amesema Edward.
Kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga amesema bado ofisi yake haijapata taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo.
“Ngoja niwasiliane na wenzangu waliopo ofisini muda huu wawasiliane na ubalozi wetu nchini humo kwa maelezo zaidi, kama limetokea pia lazima wakusanye taarifa za kina kabla ya kuzituma, hilo linaweza kuchelewesha kutufikishia taarifa mapema,” amesema Balozi Mahiga.
Chanzo na Mwananchi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo