WIMBI la viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), limezidi kushika kasi baada ya Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kata ya Maili Moja wilayani Kibaha, Mohamed Hashim kuhamia CCM.
Sambamba na katibu huyo wa kata, pia wanachama wengine tisa wa Chadema na ACT Wazalendo nao wamekabidhi kadi zao za uanachama kwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani, Ramadhan Maneno.
Hayo yalitokea Kongowe wilayani Kibaha wakati Maneno ambaye alikuwa akizungumza na viongozi na wanachama kushukuru kumchagua kwenye nafasi hiyo.
Maneno amesema, kwa sasa wapinzani wameshaona kwenye vyama vyao hakuna jipya, hivyo wameamua kumuunga mkono Dk John Magufuli ambaye anatatua kero na changamoto zilizokuwa zinawasumbua wananchi.
"Hiki ndicho kielelezo cha kumkubali kiongozi wetu, wao wenyewe wameona kinachofanyika wanaona hakuna haja ya kupoteza muda wao bora warudi nyumbani na kumsaidia Rais na hakuna sababu ya kumpinga," amesema.
Amesema, wanaCCM wanapaswa kukipigania chama kwa kuhakikisha wanalipa ada zao kwa wakati, kwani ili mwanachama awe hai lazima alipe ada zake ili kukiimarisha chama.
"Tuna wanachama 38,000 kwenye Mji wa Kibaha, lakini waliolipa ada ni wanachama 8,000 tu, hii si sawa lazima wanachama watakeleze jukumu lao hilo ili kujenga chama," amesema.
Amebainisha kwa sasa viongozi waendelee kuhamasisha wanachama kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za Vijiji na Mitaa mwaka 2019, ikiwa kama sehemu ya kujipima kabla ya mwaka 2020 wa uchaguzi mkuu.
Hashim amesema, ameamua kurudi CCM baada ya kuona kuwa kwenye chama hicho hakuna demokrasia ya kweli na kujaa malumbano ambayo hayana tija kwa wananchi.
IMEANDIKWA NA JOHN GAGARINI, KIBAHA
