Sheria ya ndoa kero Shinyanga

BAADHI ya wananchi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamedai kukerwa na Sheria ya ndoa ya mwaka 1971, inayoruhusu mtoto wa miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya mahakama na wazazi wake, hali ambayo imeonekana kuwa kichocheo kwa mimba na ndoa za utotoni.
Wameyasema sheria hiyo imekuwa mwiba, hususan pale wanapokuwa wakipambana kutokomeza vitendo hivyo, kukamata watu wanaoendekeza utamaduni wa kuozesha watoto na kuwakatisha masomo yao, ambapo sheria hiyo imekuwa kama kinga kwao.
Wameyasema hayo wakati wa utoaji elimu na kujengewa uwezo wa jinsi ya kutokomeza mila na desturi kandamizi ndani ya familia kutoka Shirika la Agape.
Mmoja wa wananchi walioshiriki, Hassani Jafari alisema sheria hiyo inatakiwa ifanyiwe marekebisho ya haraka, vinginevyo suala la kumaliza tatizo la mimba na ndoa za utotoni halitakoma, ambapo wazazi wengi kwa sasa hiyo ndiyo imekuwa kinga kwao, kuendekeza kuwaozesha watoto wadogo kwa tamaa ya kupata mifugo.
Mkurugenzi wa Shirika hilo la Agape, John Myola amesema wao walishapiga kelele juu ya kubadilishwa sheria hiyo ya ndoa, lakini serikali haijaweza kufanikiwa kubadilisha sheria hiyo.
Mpaka sasa Agape, wanatekeleza utoaji elimu hiyo kwenye Kata 12 wilayani Kishapu ambazo ni Somagedi, Laghana, Ngofila, Talahga, Itilima, Bunambiu, Mwamashele, Shagihilu, Mwamalasa, Masanga, Kiloleli na Mwakiponya. Wanatarajia kuwafikia watu 42,500.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo