Mwanamke mmoja anayejulikana kwa jina la Halima Salum (51) ambaye pia ni diwani wa Fuoni Unguja, amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuwauzia watu ardhi ya serikali na kuwatapeli fedha zao kutokana na watu hao kushindwa kuitumia ardhi hiyo kwani ni mali ya Serikali.
Akithibitisha kukamatwa kwa mwanamke huyo Kamanda wa polisi mkoa wa mjini magharibi Unguja Hassan Nassir amesema walimkamata akiwa na mwenzake aliyejulikana kwa jina la Idrisa Mwinyi Khamiss ambao kwa pamoja waliuza kipande cha ardhi huko Fuoni Kibondeni kwa Tsh. 6,000,000 ambapo mnunuzi alishindwa kufanya shughuli yeyote katika eneo hilo baada ya kubaini kuwa ni eneo la Serikali.
Wakati mwanamke huyo akiwa mikononi mwa polisi kwa upelelezi alitokea kijana Salum Saleh (28) naye pia alitoa malalamiko kwa polisi kuwa mwanamke huyo alimuuzia kipande cha ardhi ambacho si mali yake wala ya Serikali kwa zaidi ya Tsh. 2,000,000.
Katika kuitikia wito wa Serikali kutaka kuondoa migogoro ya ardhi nchini Kamanda Nassir amesema hawatosita kumchukulia hatua mwanamke huyo bila kujali cheo chake ili kutokomeza migogoro ya ardhi nchini.
