MWANAMKE aliyeshtakiwa kwa wizi mtoto pacha mwenye umri wa wiki mbili katika hospitali kuu ya Kenyatta (KNH) siku 12 zilizopita ameshtakiwa kwa wizi wa watoto wawili wachanga.
Edinah Kemunto Mabuka, ameshtakiwa kwa wizi wa mtoto huyo wa wiki kutoka kwa baba yake na mwingine wa wiki moja aliyedaiwa alimwiba miaka mitatu iliyopita.
Mabuka mwenye umri wa miaka 29 anayefanya kazi ya ujakazi alikanusha mashtaka ya kuwaiba watoto alipofikishwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi.
Alikanusha kwamba alimwiba mtoto huyo wa wiki mbili mnamo Feburuari 18 na kukamatwa naye baada ya siku mbili katika mtaa wa Kawangware.
Shtaka la pili lilisema Kemunto alimwiba mtoto wa wiki moja mnamo Septemba 22, 2015, katika eneo la OTC Kamkunji kaunti ya Nairobi kutoka kwa mama yake Bi Caroline King’ori.
“Naomba korti iamuru mshtakiwa azuiliwe kwa siku tatu kuwezesha Polisi kusafiri naye hadi mkoa wa kati kuwasaidia katika uchunguzi utakaochukua siku tatu,” kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha aliomba.
Bw Naulikha alisema mtambo wa kompyuta aliotumia afisa anayechunguza kesi hiyo uliharibika kabla ya kuchapisha nakala za afidaviti aliyotazamia kutumia kuomba mshtakiwa azuiliwe kwa siku nyingine tatu.
Ombi hilo lilikataliwa na wakili James Njengo aliyesema tangu Februari 18, polisi wamekuwa wamemzuilia mshtakiwa.
“Hakuna sababu ya kuendelea kumzuilia mshtakiwa kwa siku nyingine tatu,” alisema Bw Njengo.
Alisema polisi wangelikuwa wamekamilisha mahojiano yao na uchunguzi.
“Kumzuilia mshtakiwa zaidi ni kukandamiza haki zake sasa. Naomba korti imwachilie kwa dhamana,” alisema Bw Njengo.
Akitoa uamuzi Bw Andayi alisema mshtakiwa hatazuiliwa zaidi kwa vile amekuwa mikononi mwa polisi kwa siku 13 kufikia Ijumaa.
“Kama ni uchunguzi wangelikuwa wamekamilisha,” alisema Bw Andayi na kumwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh300,000 kwa kila kesi.
Kwa jumla atalipa Sh600,000 ndipo atoke.
“Ikiwa mshtakiwa atalipa dhamana hiyo naamuru afike kwa afisa anayechunguza kesi hiyo kila siku hadi Machi 6, 2018.
Ikiwa hatalipa basi atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga hadi alipe na akishindwa apelekwa gereza la Langata hadi Aprili 3, 2018 kesi zitakaposikizwa,” aliamuru Bw Andayi.
Na RICHARD MUNGUTI
Na RICHARD MUNGUTI
