Mbowe ametoa tamko hilo leo wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya CHADEMA eneo la Magomeni, jijini Dar es Salaam na kusema alivyokuwa mkoani Morogoro amepokea maoni mengi kutoka kwa wananchi pamoja na wanachama wa chadema ambao walitaka chama hicho kitoe msimamo wake juu ya vitendo vinavyoendelea nchini hasa hasa masuala ya mauaji.
"Jana tulivyokuwa Ifakara mkoani Morogoro wanachadema na wananchi waliomba chama kitoe tamko la kutaka kulipiza kisasi juu ya mauaji yanayoendelea kutokea. Mnaweza mkaona sasa wananchi uvumilivu umewafika mwisho, mimi binafsi kama kiongozi niliwaambia siwezi nikaruhusu kulipiza visasi kwa sababu tunahitaji kuishi kama taifa linalo heshimiana", amesema Mbowe.
Pamoja na hayo, Mbowe ameendelea kwa kusema "nimewambia viongozi wenzangu na wanachadema tusifike huko kwenye kulipiza kisasi kwa kisasi kwa sababu roho ya mtanzania yeyote bila ya kujali ni chama gani ina thamani kubwa katika maisha yetu. Tusianze kuuwana na kuchafuana wananchi kwa wananchi wenyewe. Kwa hiyo nawataka wanachama wa chadema waendelee kuwa makini kama vile viongozi wangu mbalimbali wamesema katika nyakati tofauti na tuchukue kila aina ya tahadhari".
Kwa upande mwingine, Mbowe amedai vyama vya upinzani hasa hasa CHADEMA kwa sasa wamekuwa hawapewi ulinzi na Jeshi la Polisi na matokeo yake wanawachukuliwa kama watu ambao sio raia wenye haki katika taifa hili la Tanzania.
