Taarifa hiyo kutoka ubalozi wa Marekani kwa vyombo vya habari imesema kwamba tukio hilo la mauaji la makabiliano ya kihasama na vitendo vya kikatili ni jambo linalotia wasiwasi na kusikitisha sana.
‘’Tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia na marafiki wa marehemu kwa msiba huu. Tunatoa wito kwa vyama vyote kulinda amani na usalama wa mchakato wa kidemokrasia, taifa na wa watu wa Tanzania’ ’imesema taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo imeongeza kwamba ‘’Tunaungana na Watanzania katika kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wenye uwazi ili kuwawajibisha wale wote wanaohusika na vitendo hivi vya kikatili kwa mujibu wa sheria za Tanzania".
Kiongozi wa CHADEMA kata ya Hananasif Kinondoni, Daniel John ameuawa kwa kukatwa mapanga baada ya kuamriwa kuingia kwenye gari na baadaye mwili wake kuokotwa kwenye ufukwe wa ,Coco Beach' ukiwa umekatwa mapanga sehemu mbalimbali.