Kamanda Mambosasa akiongea na waandisha wa habari leo kutoa tathamini ya ulinzi na usalama katika kipindi cha uchaguzi wa marudio katika jimbo la Kinondoni amesema kuwa mpaka sasa wanazo taarifa za watu ambao wameshiriki kufanya mauaji hayo.
"Jeshi la polisi kanda maalum linazo taarifa za watu walioshiriki katika mauaji ya mtu mmoja ambaye mwili wake uliokotwa na baadaye kujulikana kwamba ni ndugu Daniel John Mwenyekiti wa Kata ya Hananasifu ambaye mwili wake uliokotwa ukiwa umetupwa maeno ya fukwe za Coco beach, taarifa bahati nzuri tumeletewa na watoa taarifa wakielezea sakata zima la mauaji haya yalivyofanyika na kwa sababu tayari tunazo taarifa tunaendelea kufuatilia ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa ili waweze kuhojiwa na kufikishwa kwenye vyombo vya mahakama kujibu tuhuma ambazo zinaendelea" alisema Mambosasa
Aidha Mambosasa amewaomba Watanzania wawe wavumilivu na kusema kuwa tukio hilo ni tukio la mauaji kama yalivyo mengine hivyo haki itatendeka kwani kwenye taratibu za upelelezi hakuna 'double standard' bali zinafuatwa taratibu na miongozo iliyopo kwenye masuala ya upelelezi.
Februari 14, 2018 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alitoa taarifa juu ya kuuawa kwa kiongozi huyo wa CHADEMA ambaye mwili wake ulikutwa ukiwa na majeraha mbalimbali mwilini.
