Atangaza Kuwauza watoto wake Ili alipe Bili ya Mochwari

KAMANDA wa Polisi katika Kaunti ya Murang’a, Naomi Ichami Alhamisi alitoa onyo kwa mzee mmoja wa eneo hilo asithubutu kuuza watoto wake kama kwa kisingizo kuwa anataka kulipa bili ya hospitali ili maiti ya mkewe iachiliwe.
Ichami amesema kuwa haki za watoto ni lazima zilindwe kwa vyovyote vile na akamtaka Peter Njoroge, 65 atafute mbinu nyingine ya kukusanya Sh1.8 milioni anazohitaji ili alipe bili hiyo

"Tunafuatilia na ikiwa atatekeleza wazo hilo lake, basi awe tayari kujua kuwa watoto ni wa serikali, yeye kazi yake ni kuwahifadhi katika boma lake,” alisema Ichami.
Njoroge tayari amesema kuwa anawazia kuwachuuza watoto wake watatu wa chini ya umri wa miaka 15, shamba lake la ekari moja na pia ng’ombe wa familia ili kupata afueni ya bili hiyo.
Mzee huyo wa imani ya Akorino ambaye ni wa kutoka kijiji cha Kaganda katika Kaunti ndogo ya Kiharu amesisimua wenyeji kwa hisia mseto kufuatia tangazo hilo lake.
Amesema kuwa sasa ni miezi minne tangu bibi yake, Lucy Wairimu aage dunia akiwa amelazwa hospitalini na akatwikwa bili ya Sh1.8 milioni ambazo hajaweza kupata licha ya kuandaa harambee kadhaa ambazo zimefanikiwa kupata Sh100,000 pekee.
Wiki jana wakati Naibu Rais William Ruto alizuru Kaunti za Kiambu na Murang’a, mzee huyu alijaribu kumfikia ili amweleze masaibu yake lakini ulinzi mkali alioandamana nao ukamzima katika jitihada hizo.
Ichami anamtaka mzee huyo ajaribu kuwasilisha malalamishi yake rasmi kwa afisi za serikali na pia katika afisi za viongozi wa eneo hilo.
“Mimi mwenyewe nimeuliza nyanjani kama mzee huyu amefahamisha diwani wake, mbunge, mwakilishi wa wanawake, Seneta na Gavana kuhusu hali yake ya mahangaiko. Jibu nimepata kuwa hajafanya hivyo,” akasema.
Alisema kuwa afisi ya Kamishna wa Kaunti pia inaweza ikashughulikia suala hilo lakini yeye amerukia wazo lililo kinyume kabisa na sheria na anafikiria 'tutamshangilia'.
Ichami amesema kuwa kuuza watoto ni uhalifu wa kimataifa kwa kuwa unaorodheshwa miongoni mwa hatia kuu za ulanguzi, hilo lake likiwa ni ulanguzi wa binadamu.
Hata hivyo, Njoroge ameshikilia kuwa yeye anajaribu tu kujipa afueni kulingana na rasilimali ambazo amepewa kama Baraka na mwenyezi Mungu na kamwe hatakubali kushurutisghwa atupilie mbali mradi huo wake ikiwa hakuna anayempa afueni.
Amesema kuwa bili hiyo katika hospitali kuu ya Kenyatta imemhangaisha vya kutosha ikizingatiwa kuwa atalipa kwa huduma ambazo ziliishia kumpokonya mke kwa mkuki wa mauti.
Amesema kuwa hatachoka kujaribu kila mbinu ya kujikomboa kutoka hali ya sasa ambapo “mwili wa mpendwa wangu wa kimaisha unaendelea kulala kwa jokovu katika hospitali ya umma ambapo hakuna usiri badala ya kuwa hapa shambani mwangu katika usiri wake ndani ya kaburi.”


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo