Hayo yamesemwa leo na kiongozi wa Chama hicho Mh. Zitto Kabwe ambaye amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kufanya tathmini ya uchaguzi mdogo wa Udiwani uliofanyika katika Kata 43 na kugundua kuwa haukuwa huru na wa haki.
“Chama Cha ACT Wazalendo kimeshiriki katika uchaguzi kwenye Kata 43 na kimeshuhudia hali mbaya yakutokuwa na uwanja sawa wa ushiriki wa Uchaguzi na kwa kupitia vikao vyake halali vya kikatiba, Chama kimeonelea kwamba mazingira ya kushiriki kwenye uchaguzi sio sawa”, amesema Zitto.
Aidha Mh. Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini ameongeza kuwa chama chake kimeagiza kuanza mazungumzo na vyama vingine vya upinzani kwaajili ya kuanza kuweka mashinikizo ya kufanya mabadiliko muhimu yanayotakiwa kwenye sheria. Pia ameweka wazi kuwa chama chake hakijajiunga wala hakijashirikiana na UKAWA katika maamuzi yake.
“Tumemwagiza Katibu mkuu wa chama aitishe kikao cha makatibu wakuu wa vyama vingine vya upinzani ili kuanza mikakati ya pamoja ya kushughulikia jambo hili”, ameongeza. Uchaguzi huo unahusisha majimbo matatu ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido.