Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo Naibu Mkurugenzi wa TAKUKURU Brigadier General John Mbungo amesema mtu huyo awali alianza kuonyesha ushirikiano walipoanza kumuhoji, lakini baada ya muda akaanza kuwakwepa na hatimaye kutokomea kusikojulikana.
"Tumeendelea kumtafuta na taarifa tulizozipata amekuwa anakimbia nchi kupitia njia ambazo sio rasmi na hadi sasa tumeendelea kumtafuta lakini bado hajapatikana. Na sisi tumeona ni vema tuziweke hizi habari ziwe wazi kwenu waandishi wa habari na wananchi, popote watakapompata au kumuona huyu bwana watoe taarifa katika chombo hiki na taasisi hiii itamzawadia mtu yeyote ambaye atafanikisha kupatikana kwa huyu mtu, zawadi ya milioni 10 pesa taslim.", amesema Brigadia Mbungo.
Godfrey Gugai alikuwa mhasibu wa TAKUKURU anatuhumiwa kuwa na mali nyingi kinyume na sheria kwa mtumishi wa umma, ambapo ana nyumba ya ghorofa 4 iliyopo Ununio Knondoni, nyumba ya ghorofa 3 Bunju, ana nyumba za kupangishwa Mbweni, ana nyumba za kupangisha Kinondoni, ana jengo la kifahari Majita Musoma, ana nyumba Mwanza, ana nyumba ya kifahari Mwanza Nyegezi, ana viwanja lukuki sehemu mbali mbali na mali nyinginezo.