Mbunge wa CHADEMA mbaroni kwa kuchoma moto shule

Polisi mkoani Morogoro inawashikilia watu 41 akiwemo mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga, madiwani wawili kwa madai ya  kufanya fujo na kuchoma moto majengo ya shule baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Sofi wilayani Malinyi.

Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei amesema tukio hilo lilitokea jana Jumapili Novemba 26, saa tano usiku ambapo walikwenda kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa udiwani.
Kamanda Matei amesema wabunge hao na madiwani wawili wa Chadema kutoka Ifakara walionekana kuhamasisha baadhi ya wafuasi wao kufanya vurugu.
Kamanda Matei amesema fujo na uharibu huo ulitokea baada ya msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo kuwa mgombea wa CCM ndiye alishinda kwa kupata kura 2,099 na mgombea wa Chadema kupata kura 1,684 jambo lililopingwa na wafuasi wa chama hicho na kuanza vurugu.
Amesema watuhumiwa wanadaiwa kuchoma majengo ya umma ambayo ni ofisi shule ya msingi Sofi, nyumba ya walimu wa shule hiyo na ofisi ya mtendaji kata na kwamba baada ya kuchoma majengo hayo kwa kutumia petroli, walidhamiria pia kwenda katika zahanati lakini askari waliwakamata.
"Wakati sisi tukipambana na vitendo vya uhalifu na kudumisha amani wao wanateketeza mali za umma ambazo zinatumiwa na watanzania masikini kabisa, wanaosoma kwenye shule hizo ni watoto wa wakulima, hatuwezi kukubali. Huu ni uhalifu" Kamanda Matei.
Aidha Kamanda Matei amesema kwamba watuhumiwa hao bado wapo chini ya ulinzi na wamepelekwa wilayani Ulanga kwa ajili ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Hata hivyo polisi inaendelea kuwatafuta watu wengine waliohusika na vurugu hizo, akiwemo Mbunge Peter Lijualikali.



JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo