Shamba la Manji Lililofutwa umiliki lafyekwa



wananchi wa Kigamboni wakiongozwa na Viongozi wa wilaya wamejitokeza na kufyeka pori la NAFCO lililoko kata ya Somangila. 

Pori hilo ambalo awali lilikuwa likimilikiwa na mfanyabiashara Yusuph Manji ambaye alishindwa kuliendeleza, lilikuwa hatarishi kwa usalama wa eneo hilo na wapita njia hasa muda wa usiku. 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mhe Hashim Mgandilwa amewashukuru wananchi kwa kuwa watulivu muda wote ambao walikuwa wakilalamikia pori hilo huku serikali ikiwataka wawe na subira wakati taratibu za ufutaji zinaendelea. 

DC Mgandilwa pia amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ni sikuvu inayodhamiria kuleta maendeleo kwa wananchi. 

"....serikali yenu ni sikivu sana,..... Ndiyo maana Rais Magufuli amesikia kilio chenu na kuamua kuifuta hati ya Shamba hili ili liwe mikononi mwa serikali.....,tuendelee kuiunga mkono serikali na sitaki kuona mtu anafanya siasa katika hili....TUFANYE KAZI... " alisisitiza DC Mgandilwa.

Aidha amewapa wananchi wiki moja kuanzia leo kuendelea kusafisha eneo hilo kwa kufyeka vichaka na kukata miti kwa matumizi yao ya nyumbani kama kuni au shughuli za ujenzi. 

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Mhe Dkt Faustine Ndungulile, amewataka wananchi kuendelea kushikamana kwa Umoja katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwani Kigamboni itajengwa na wote.

Pia Dkt Ndungulile amewaomba wananchi waendelee kuiunga mkono serikali yao kwani imetatua kero zao kubwa ikiwemo Rais Magufuli kuifuta mamlaka ya Uendelezaji wa Mji wa Kigamboni (KDA) ambayo ameipigia kelele kwa muda mrefu bungeni. 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Ndg Stephen Katemba amesema kuwa eneo hilo lisivamiwe na mtu yeyote kwa shughuli zake binafsi iwe kujenga au kulima kwani hapo ndipo inatarajiwa kujengwa Makao Makuu ya Wilaya.

Shughuli za ufyekeji pori hilo zimeanza mapema alfajili na kuhudhuliwa na Viongozi wa wilaya, Mbunge, Wahe Madiwani,   watumishi wa manispaa ya Kigamboni na wananchi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo