Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji
Jumla ya wanafunzi wa kike nane wa shule za sekondari na saba na shule za msingi wilayani Rufiji mkoani Pwani ,wamebainika kuwa wana mimba, mwaka huu. Kutokana na taarifa hiyo, mkuu wa wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo, amewaasa wanafunzi wa kike kuacha kukimbilia mambo ya ovyo badala yake wajidhatiti katika elimu ili kupata maarifa na ufahamu.
Akizungumza baada ya kukamilisha ziara yake ya mwezi mmoja ya kutembelea shule 43, kuzungumza na wazazi na walezi, alisema mimba za utotoni zinakwamisha jitihada za kumkomboa mtoto wa kike kitaaluma. Njwayo alieleza, kati ya mimba zilizobainika mwanafunzi mmoja ni wa shule ya sekondari Ngorongo, Nambunju na wengine saba ni wa shule za msingi.
Alifafanua, zipo hatua za kisheria zinazochukuliwa kwa waliohusishwa kuwatia mimba wanafunzi hao, ambapo watendaji wa kata wameshawashtaki kwenye vyombo vya sheria. Alisema, pia wanatengeneza mazingira mazuri kwa watoto mashuleni kwa kuwataka walimu wakae nao mara kwa mara kuwaelimisha wajiepushe na wanaume wadanganyifu .
Kwa mujibu wa Njwayo, kilichomsukuma kufanya ziara hiyo ilikuwa baada ya kupata taarifa kuwa kuna wanafunzi watoro wa kudumu 190 kati ya wanafunzi 2,442 wanaotarajiwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu. Aidha katika ziara hiyo amefanikiwa kuwarejesha shule wanafunzi hao 54 wa shule ya Ikwiriri, shule ya msingi Utete tisa na shule ya msingi Mapinduzi tisa.
Njwayo alielezea, alichogundua ipo changamoto ya wazazi kutokuwa na ushirikiano na walimu na kutofuatilia mwenendo wa watoto wao kila siku.
"Elimu ni muhimu, ni nguzo na msingi wa maisha yetu, na kwa watoto wetu, itaweza kuwasaidia kupata ufahamu wa kujiajiri na kuwa mwanakilimo bora wa kisasa na kuwa na upeo kuliko kukosa elimu " alisisitiza Njwayo.
Njwayo ,alisema kwasasa kuna watendaji wa vijiji na kata wamefukuzwa kutokana na kukatwa kwani hawakuwa na cheti cha kidato cha nne hivyo wanaajiriwa wapya kuziba mapengo .
"Hapo ndipo inapoonekana thamani ya elimu ,hivyo wanafunzi waache michezo na vishawishi ,;wasome kwa bidii " alisema Njwayo.