Msichana ajiua baada ya mwalimu kumtoa darasani kisa damu ya ‘HEDHI’

Msichana wa umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi kusini mwa India amejiua baada ya mwalimu wake kumuaibisha kwa sababu ya hedhi  na kuacha ujumbe wakati wa kujiua, alidai mwalimu wake “alimtesa”.

Ingawa msichana huyo hakutaja kisa hicho cha kuaibishwa kwa sababu ya hedhi, mama wa msichana huyo anasema aliagizwa na mwalimu wake kutoka nje ya darasa kwa sababu ya doa la damu ya hedhi lililokuwa kwenye nguo zake.

Hedhi ni mwiko kuzungumziwa hadharani India.

Wanawake kitamaduni huaminika kuwa wachafu au hata waliolaaniwa wakati wanapopata hedhi.

Polisi wanasema wamepata ripoti za kisa hicho cha kujiua kilichotokea katika wilaya ya Tirunelveli siku ya Jumapili katika jimbo la Tamil Nadu, na hadi sasa wanaendelea kufanya uchunguzi.

“Sijui ni kwa nini mwalimu wangu analalamika kunihusu. Bado sielewi ni kwa nini ananihangaisha na kunitesa hivi,” mwanafunzi huo aliandika kwenye barua yake.

Alianza barua hiyo: “Amma (mama), tafadhali nisamehe.”
Mama wa mwanafunzi huyo anadai mwalimu huyo alimchapa binti yake siku za awali kwa kutofanya kazi yake ya ziada.

“Binti yangu alipata hedhi akiwa shuleni Jumamosi iliyopita,” mamaake ameambia BBC Tamil.

“Alipomjulisha mwalimu wake, alipewa kitambaa cha kupangusa ubao atumie kama sodo.

“Mwalimu alimfanya binti yangu kusimama nje ya darasa. Msichana wa miaka 12 atavumiliaje aibu ya aina hiyo?” alishangaa.

Msichana huyo alijiua siku moja baadaye.

Shule hiyo imeiambia BBC kwamba inashirikiana na polisi katika uchunguzi.
Chanzo-BBC


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo