Manara amebainisha hayo baada ya kupita siku chache tokea mkutano mkuu wa wekundu wa Msimbazi kupitisha maamuzi ya kubadilisha umiliki wake kutoka klabu ya michezo inayomilikiwa na wanachama mpaka kuwa kampuni inayomilikiwa na wanahisa.
"Kamati ya utendaji ilikutana hivi karibuni na kuamua kuunda kamati ya kupitia mchakato wa zabuni wa kumpata mwekezaji au wawekezaji ambao ni wanachama wa Simba, watakaonunua hadi asilimia 50 ya hisa za klabu ya Simba. Katika zile asilimia 100, asilimia 50 zinapaswa ziuzwe kwa mwanachama wa Simba kwa mfumo wa tenda ambao kamati itakayosimamia shughuli hiyo imeshaundwa na leo ninaitangaza kamati hiyo ambayo itakuwa huru na haitaingiliwa katika mchakato huu. Uuzwaji huo utafanyika kwa kuzingatia sheria za nchi, tuna imani kubwa na timu hii tuliyoiunda kwa sababu ina watu wabobezi," alisema Manara.
Pamoja na hayo, Manara amewataka wanachama wa Simba wajitokeze kwenda kununua hisa hizo baada ya kutoka kwa matangazo yatakayorushwa katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Kwa upande mwingine, Kamati ya Utendaji wa Klabu ya Simba imewateua wajumbe watano ambao wataongozwa na Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu Thomas Mihayo, Wakili Damas Ndumbaro, Mbunge wa Ilala Musa Azzan 'Zungu', Abdulrazack Badru ambaye ni Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini pamoja na mtaalamu wa manunuzi Yusuph Majid Nassoro.