Imeelezwa kuwa maamuzi hayo yamefikiwa ili kuokoa nguvu kazi ya taifa ambayo imeathiriwa kwa kiasi kikubwa kutokana na watu wengi nchini humo kuendekeza masuala ya ngono.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maadili wa Uganda, Simon Lokodo, tume hiyo itakayokuwa na wajumbe tisa na watalaam wengine kati ya 30 hadi 40 itatengewa bajeti ya Shilingi Bilioni 2 kila mwaka.
Bw. Lokodo amefafanua kwamba, tume hiyo itakuwa na vifaa vya kisasa kuingilia watu wanaohusika na kusambaza, kupakua, na kuangalia picha na video za ngono kisha kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Amedai kuwa vitendo hivyo vinaliangamiza taifa hilo kwa kuchochea ongezeko la mimba za utotoni, matumizi ya dawa za kulevya, ushoga na ubakaji.