Kamanda Mambosasa ametoa wito huo leo wakati alipokuwa anajitambulisha mbele za waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam mara baada ya kukubali kuitikia wito wa uteuzi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Nyakoro Sirro aliyeufanya Agosti 24 mwaka huu.
"Mimi niwaalike wakazi wa Dar es Salaam wote kuwa kila mtu amwangalie mwenzake katika masuala ya uhalifu, ila suala la utekaji nyara watu mkiwa mnafikiria ni tatizo la jeshi la polisi pekee yake mtakuwa mnakosea. Kila mmoja wetu anaweza akawa mtekwaji mtarajiwa kwa hiyo tusikubaliane na uhalifu tuwafichue hao watu", alisema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa aliendelea kwa kusema "mkiwafichua nileteeni taarifa na ikifika kwangu nitawachukulia hatua za haraka kwa hao ambao wamekuja kuripotiwa kuwa ni wahalifu. Nitahakikisha Dar es Salaam siyo mahali pakuzalishia uhalifu"
Pamoja na hayo, Kamanda Mambosasa amedai siku zote katika utendaji kazi wake huwa anaamini kazi nzuri ni ile yenye kuwashirikisha watu.
"Ni jambo baya la kumpuuza mtu kwa maana huyo huwenda akawa ndiyo mwenye taarifa ambayo ingesaidia katika kuzuia uhalifu kwa hiyo nitaitumia jamii, vijana wangu kwa maana maafisa wakaguzi, Makamanda wa polisi wa mikoa yote ndani ya Jiji la Dar es Salaam", alisisitiza Kamanda Mambosasa.
Kwa upande mwingine, Kamanda Mambosasa amesema Dar es Salaam ni mkoa mkubwa kuliko mingine hivyo atahakikisha mkoa aliyokabidhiwa wa Dar es Salaam kutokuwa maficho ya uhalifu kwa watu wanaotenda uhalifu pembezoni na kukimbilia Dar es Salaam hivyo amedai hawatabaki salama.