Aliyekuwa waziri mkuu nchini Tanzania na mgombea wa urais katika chama cha upinzani Chadema katika uchaguzi uliopita Edward Lowassa amewataka Wakenya kuvumiliana wakati huu ambapo taifa hilo linakaribia uchaguzi.
Akizungumza nchini Kenya katika mazishi ya aliyekuwa waziri wa usalama nchini humo marehemu Joseph Nkaiserry, Lowassa amesema kuwa kenya inapaswa kujifunza kutoka kwa machafuko ya uchaguzi ya mwaka 2007.
Matamshi yake yaliungwa mkono na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta aliyewataka wafuasi wake na wale wa kiongizi wa upinzani Raila Odinga kuvumiliana.
Uhuru alisema kuwa hakuna haja ya kupakana tope za matusi akiongezea kuwa matusi hayasaidii.
''Sisi sote ni Wakenya , hatuna taifa jingine la kujenga baada ya uchaguzi ,tunaomba amani, amani amani'', alisema rais Uhuru Kenyatta.
Matamshi ya Uhuru na Lowassa yanajiri wakati ambapo wafuasi wa upinzani na wale wanaounga mkono serikali wamekuwa wakiwazomea viongozi wanaotoka pande pinzani katika mikutano ya kampeni na hata kusababisha mikutano hiyo kusitishwa.
Lowassa amesema kuwa Kenya ni tegemio la kiuchumi katika mataifa ya Afrika mashariki hivyobasi inafaa kuwa mfano kwa kuhakikisha kuwa taifa hili halijiingizi tena katika jinamizi la machafuko yalioonekana miaka 10 iliopita.
''Ombeni musirudi katika mapigano yaliotokea mwaka 2007, Kenya iko mbele kushinda taifa lolote lile Afrika mashariki na tunataka muendelee kusonga mbele.
Lowasa alisema kuwa marehemu Nkaissery aliamini sana Umoja wa Afrika mashariki na alijitolea kufanya kazi na akawataka viongozi wengine kuiga mfano wake.
Naye rais Uhuru aliongezea kwamba Kenya na Tanzania ni pacha na zitaendelea kuimarisha ushirikiano wao kwa lengo la kurahisisha biashara na usalama kati ya raia wa mataifa hayo mawili.
Miongoni mwa wale waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga na naibu wa rais William Ruto