Mkuu wa wilaya ya Liwale,mhe. Sarah Chiwamba wa pili kutoka kushoto akimpatia mototo chanjo (picha na Mwandae Mchungulike).
Afisa maendeleo ya jamii wilaya ya Liwale,Mary Ling'oh akitoa neno katika uzinduzi wa chanjo leo aprili 24
Miongoni mwa akina mama walioudhulia kwenye uzinduzi wa chanjo uliofanyika katika hospitali ya wilaya ya Liwale.
Na Mwandae Mchungulike,Liwale
Mkuu wa wilaya ya Liwale Mheshimiwa Sarah Chiwamba amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Liwale kutowaficha watoto wao na badala yake wawapeleke kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupata chanjo.
Mheshimiwa Chiwamba ameyasema hayo leo Aprili 24 alipokuwa akizindua amezindua siku ya chanjo kwa watoto katika hospitali ya wilaya Liwale.
“Ndugu zangu tubadilike na tuachane nay ale mazoea ya kutowapeleka watoto wetu hospitali kwa ajili ya chanjo. Hizi chanjo ni muhimu sana kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya aina mbalimbali kwa watoto wachanga” Alisema mheshimiwa Chiwamba.
Akizungumza kwa niaba ya akina mama waliohudhuria kwenye zoezi hilo, Bi. Doto Alawi amesema jamii inatakiwa kutambua na kuthamini umuhimu wa chanjo kwa watoto kwani inamkinga mtoto dhidi ya magonjwa yanayokingika. Pia aliwahamasisha akina mama wengine kujitokeza kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya kupatiwa chanjo.
Zoezi hilo la chanjo limeanza Aprili 24 na litaendelea hadi Aprili 30 mwaka huu na likiwa limebeba kauli mbiu isemayo “Jamii iliyochanjwa ni jamii yenye afya”