MWANAMUME mmoja Mwingereza amefungwa jela miaka 21 kwa makosa 13, moja la kubaka mtoto wake wa kike, ambaye ni msagaji, ‘kumfundisha kuwa ngono inastahili kuwa kati ya mume na mke.’
Tovuti ya Stuff, ambayo imenukuu gazeti la The Mirror, imesema kuwa mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 54 alishambulia mtoto wake mwenye umri wa miaka 16 alipomwambia kuwa anavutiwa kimapenzi na wanawake pekee.
Jaji Andrew Lockhart QC alisema mahakamani, “Ulionyesha kuwa huwezi kudhibiti hasira yako na ukaamua kumbaka ili kumuonyesha kuwa ingekuwa bora zaidi kama angefanya mapenzi na wanaume kuliko wanawake. Ushahidi wake ulitisha kusikiza.'
“Ubakaji huo ulimshusha hadhi na kumdhalilisha. Kosa hilo lilionyesha wazi uadui ulionao kwake kwa kuwa shoga.”
Iliripotiwa kuwa mwanamume huyo pia alidhulumu kimapenzi mtoto wake mwingine wa kike kwa zaidi ya miongo miwili.
Alisukumwa jela miaka 21 baada ya kupatikana na makosa matatu ya ubakaji miaka ya 1980 na 1990, makosa tisa ya kufanya matendo yasio na heshima na moja ya kufanyia mtoto matendo machafu.
Akitoka jela, atatumikia kifungo cha nje cha miaka mingine mitano ili kuhakikisha anatangamana na jamii na pia harudii makosa hayo tena.
Imekusanywa na GEOFFREY ANENE