MAKETE
Walimu waliostaafu 24 mwaka huu wilayani Makete mkoani
Njombe wameshauriwa kuwa makini na matumizi ya fedha za mafao wanazozipata
kwani zimelenga kuwasaidia baada ya kustaafu
Kauli hiyo imetolewa jana na mgeni rasmi ambaye pia ni
Afisa elimu Msingi wilaya ya Makete Anton Mpiluka katika hafla ya kuwakabidhi
zawadi ya bati 20 kila mmoja za futi 10 geji 30 wastaafu hao iliyofanyika
katika ukumbi wa Spiritual Makete mjini
Mpiluka amesema kwa kuangalia kwa macho fedha za mafao ya
kustaafu huonekana ni nyingi lakini linapokuja suala la matumizi yasiyo mazuri
fedha hizo hazitoshelezi
Amewataka walimu hao wastafu kuwa karibu na familia zao
katika kipindi hiki pamoja na kubuni miradi ambayo wataweza kuimudu kuisimamia
na itakuwa na manufaa kwao huku akiongeza kuwa kustaafu kwao kumesababisha
upungufu mkubwa wa walimu katika wilaya ya Makete
Akitoa taarifa fupi katika hafla hiyo Katibu wa Chama cha
Walimu (CWT) Wilaya ya Makete Mwl Elizabeth Petro ameikumbusha serikali
kuendelea kutatua kwa jicho la kipekee changamoto za walimu wastaafu ikiwemo
kuchelewesha kuwapatia mafao yao kwa muda mrefu, pamoja na waajiri kushindwa
kuwasafirisha makwao pindi wanapostaafu
Kwa upande wake mwenyekiti wa CWT wilaya ya Makete Mwl
Thobias Kasambala amewakumbusha walimu kwa ujumla kuzingatia maadili ya taaluma
ya ualimu, pamoja na kulipongeza baraza kuu la CWT Taifa kwa kukubali ombi la
kuwapa zawadi walimu wastaafu nchini kote ambao ni wanachama wa chama hicho
Baadhi ya wageni waliopata nafasi ya kuzungumza katika
hafla hiyo akiwemo mwakilishi wa TSC Orgen Sanga na afisa elimu sekondari
wilaya ya Makete Jacob Meena wamewasihi wastaafu hao kutojiingiza katika siasa
kama wagombea, pamoja na kutoacha ualimu wao uelee hewani hata kama
wameshastaafu wakubali kushauri ama kufundisha kwa kujitolea pale inapobidi
Wastaafu hao wakizungumza na mwandishi wetu wameahidi
kuyafanyia kazi yale yote waliyoambiwa ili uwepo wao katika jamii uzidi
kuonekana
Jumla ya wastaafu 24 wakiwemo 23 wa shule za msingi na 1
wa shule ya sekondari wamekabidhiwa zawadi hizo ikiwa ni awamu ya pili tangu
utaratibu huo uanze kutumika mwaka jana