KATIBU wa Chama cha Wanataaluma Waislamu Tanzania (TAMPRO) mkoani Shinyanga, Shomari Iddi anatuhumiwa kutaka kujimilikisha kiwanja kilichotolewa kwa ajili ya ujenzi wa msikiti eneo la Kata ya Kitangiri mjini hapa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana kwa waandishi wa habari na viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kata ya Kitangiri katika Manispaa ya Shinyanga, kiongozi huyo anadaiwa kuilaghai Idara ya Ardhi na kupewa ofa ya kumiliki kiwanja namba 1627 kitalu GG ambacho kiliishatolewa kwa Bakwata.
Mmoja wa viongozi wa Bakwata katika Kata ya Kitangiri, Hamad Masoud aliwaeleza waandishi kuwa kiongozi huyo wa TAMPRO mwaka 2007 aliwalaghai watendaji wa Idara ya Ardhi Manispaa ya Shinyanga na wakampatia ofa ya kiwanja hicho, wakiamini ni miongoni mwa viongozi wanaohusika.
“Kiwanja hiki kilitolewa na Idara ya Ardhi kwa waumini wa Kata ya Kitangiri mwaka 1994, kwa ajili ya kujenga msikiti eneo la Songambele. Hata hivyo, kabla ya viongozi wa Bakwata hatujafuatilia ofa kwa ajili ya maandalizi ya kupatiwa hati rasmi, huyo bwana (Shomari) alikwenda ardhi na kuomba apewe ofa hiyo,” alidai Masoud na kuongeza: “Tulipopata taarifa tulipinga kitendo hicho na Idara ya Ardhi iliamua kumuandikia barua yenye kumbukumbu namba SH/19260/7 ya Agosti 4, mwaka huu ikimtaka arejeshe ofa aliyokabidhiwa baada ya kubainika ilitolewa kwake kimakosa, aligoma kuirejesha na tukafungua kesi katika Baraza la Ardhi la Kata ambako tulimshinda.”
Akifafanua, Masoud alisema baada ya kushindwa katika Baraza la Ardhi la Kata, walifuatilia ili kupata uhakika iwapo kweli kiongozi huyo anatambulika na uongozi wa Tampro Makao Makuu baada ya kumtilia shaka, kwa vile mjini Shinyanga hakuna ofisi zozote za taasisi hiyo na kuhisi anatumia jina hilo kwa maslahi yake binafsi.
Alisema pamoja na kutolewa kwa maamuzi ya Baraza la Ardhi la Kata, kiongozi huyo hakutekeleza amri ya kuirejesha ofa aliyopewa na hivyo imewalazimu kwenda kukaza hukumu hiyo katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Shinyanga ili sheria imlazimishe arejeshe ofa aliyopewa kimakosa.
“Ajabu ndugu yetu huyu baada ya kusikia tumekwenda kukaza hukumu na yeye ametafuta wakili wamekwenda kuweka pingamizi kuzuia kusudio letu la kukaza hukumu, tunashangazwa na hatua yake maana tumejaribu kuwasiliana na Tampro Makao Makuu Dar es Salaam wamedai hawamtambui,” alidai Masoud.
Alieleza kuwa baada ya kuwekwa kwa pingamizi la kukaza hukumu, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya limepanga kusikiliza maombi ya kiongozi huyo Desemba 15, mwaka huu na wao wanaamini haki itatendeka baada ya kusikilizwa kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Katibu huyo wa Tampro Mkoa wa Shinyanga, Shomari Iddi amekanusha madai ya kutaka kupora kiwanja cha Bakwata na kudai wao walipewa kiwanja hicho na Idara ya Ardhi Manispaa ya Shinyanga mwaka 2007 baada ya kufuata taratibu zote za uombaji wa viwanja.
“Si kweli kwamba tumenyang’anya kiwanja cha Bakwata, hawa wenzetu wanadanganya, kiwanja hiki tuliomba kutoka idara ya ardhi kwa maombi yetu tuliyopeleka kwa barua yenye kumbukumbu namba TAMPRO/SHY/2007/1, na tulikubaliwa na kupewa ofa ya kiwanja namba 1627 block GG baada ya kulipia ada zote husika,” alidai.
“Ni kweli Bakwata walifungua kesi katika Baraza la Ardhi la Kata ya Kitangiri na shauri lilisikilizwa Septemba 27, mwaka huu, walipewa ushindi, ni baada ya shauri kusikilizwa upande mmoja, sisi hatukushiriki, tulipinga maamuzi yaliyotolewa baada ya kubaini halikuwa na uwezo wa kulisikiliza, wamekaza hukumu hiyo na sisi tumeweka pingamizi,” alieleza Iddi.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Tampro amekiri madai ya taasisi yake kutokuwa na ofisi rasmi mjini Shinyanga na kueleza kuwa hivi sasa wako mbioni kutafuta ofisi rasmi. Pia alikanusha madai ya kutotambuliwa kwa uongozi wao na Tampro Makao Makuu jijini Dar es Salaam.
Chanzo:Habarileo