Wizara ya ujenzi,uchukuzi na mawasiliano kupitia wakala wa kuhudumia barabara nchini TANROADS,imetangaza kuifunga barabara kuu ya Mwanza-Tarime hadi mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo la Sirari ili kuruhusu ukaguzi na matengenezo ya daraja kubwa la kirumi katika mto mara linalounganisha pande hizo mbili.
Taarifa ambayo imetolewa na wizara hiyo kupitia kwa kaimu meneja wa TANROADS mkoa wa Mara mhandisi Japherson Nnko,imesema daraja hilo katika mto huo unaounganisha pia ziwa Victoria, litafungwa kwa kila baada ya saa kuanzia sasa hadi desemba saba mwaka huu katika kuruhusu uchunguzi wa uimara wa waya maarufu kama cable stays kazi ambayo itafanyika kwa kutumia mionzi ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu na viumbe hai.
Hata hivyo kaimu meneja huyo wa TANROADS mkoa wa Mara,amewatahadhali wananchi wanaoishi jirani na daraja hilo kuchukua tahadhali wakati wote wa kufanya kazi hiyo maarufu kama x-ray na kwamba zoezi hilo litafanyika wakati wa mchana pekee na kuruhusu shughuli za usafirishaji kuendelea wakati wa usiku.