Bibi Harusi Mtoto aitoroka harusi yake Muda mchache Kabla ya Kuolewa

ILIKUWA Desemba, 2015. Halima Juma (si jina halisi), mwenye umri wa miaka 16, alipoingiwa na wazo la kutoroka nyumbani kukwepa ndoa ya utotoni. Binti huyo mkazi wa wilayani Kishapu katika Mkoa wa Shinyanga, alichukua uamuzi wakati harakati za sherehe za kimila zikiendelea kabla ya kuozeshwa kwa mwanaume wa kijijini kwao.
Akili ya kutoroka ilimjia akiwa mtoni, siku moja kabla ya sherehe hizo. Matangazo yaliyokuwa yakitolewa na Shirika la Agape ndiyo yaliyomzindua na kumwepusha na ndoa za utotoni.
“Nilipofika mtoni, nilisikia sauti kupitia kwenye kipaza iliyokuwa ikielezea madhara ya ndoa za utotoni. Ndipo wazo la kutoroka nyumbani kukwepa kuolewa, liliponiijia,” anasema Halima.
Anaendelea kusimulia, “Niliwaza kwa muda mrefu nifanye nini ili ndoa isifanikiwe. Siku ya mkesha wa kuamkia sherehe ya ndoa ambayo ilikuwa Ijumaa, usiku nilifikia uamuzi wa kutoroka kuelekea mjini.”
Wazazi wa Halima walifariki dunia, hivi sasa ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Agape.
Binti huyu ambaye ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto wanne, anasema, “baba alifariki mwaka 2007 na mama alifariki mwaka 2012.”
Anasimulia juu ya maisha yake na namna mlezi wake alivyoamua aache shule kwa sababu ya kukosa ada na kubaki nyumbani, kabla ya kulazimishwa kuolewa. Anasema baada ya mama yake, yeye na ndugu zake, walichukuliwa na mama yao mkubwa.
Wakati huo, dada yake mkubwa alikuwa ameshaolewa.
“Baada ya maisha kuwa magumu mama mkubwa aliamua kutupeleka kwa baba wa ukoo. Mwaka 2008 kaka yangu alifaulu alilazimika kusubiri mirathi ili kupelekwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2011. Kaka alisoma hadi kidato cha tano, fedha zilipoisha,” anaeleza.
Anasimulia zaidi, “Mimi nilipomaliza darasa la saba mwaka 2014, nilifaulu kujiunga na shule ya sekondari ya Busiya iliyopo Kishapu. Baba wa ukoo hakuwa na hela, hivyo wenzangu walianza mapema. Kutokana na fedha kukosekana, nililazimika kujiunga mwezi wa pili na mwezi mmoja baadaye nilirudishwa nyumbani kwa sababu ya ada na baba alinitaka nikae nyumbani.”
Desemba 2015 alichumbiwa na ndipo alifanikiwa kutoroka nyumbani wakati harakati za sherehe za kimila zikiendelea siku moja kabla ya ndoa. Baada ya kutoroka, akiwa njiani alikutana na mama mmoja ambaye alimuomba msaada wa kumuelekeza lilipo Shirika la Agape.
“Yule mama alinichukua na nilimweleza kila kitu,” anasema.
“Nilishangaa baadaye ndugu zangu walinifuatilia wakataka nirudishwe nyumbani lakini yule mama aliwakatalia akasema atanisomesha… hivyo yule mama alinipeleka Agape na sasa naendelea na masomo,” anasema.
Simulizi hii ya ushindi wa Halima dhidi ya ndoa za utotoni, inatajwa kuwa ni ujumbe kwa serikali na mashirika mbalimbali kuhakikisha ukatili wa kijinsia unapigwa vita. Halima anarejea kisa chake na kusema, kinatoa changamoto kwa wadau mbalimbali ikiwamo serikali, kuweka mazingira ya kuwasaidia watoto wanaokatishwa ndoto zao za elimu kwa sababu ya kulazimishwa ndoa katika umri mdogo.
“Wapo watoto wengi wanaokatishwa ndoto zao za elimu na kuolewa katika umri mdogo lakini wamekosa wa kuwasemea au pia wanakosa mbinu za kutoroka kama nilivyofanya mimi hivyo naiomba serikali ichukue hatua kwa watu wanaofanya ukatili huu,” anaeleza.
Ofisa Ustawi wa kituo cha Agape, Hellen Daudi anashauri kuifanyia kazi sheria ya ndoa kwa ajili ya kuwanusuru watoto wanaokatishwa ndoto zao za elimu na kuozeshwa kwa kuwa ni ukatili wa kijinsia. Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) ni miongoni mwa wadau ambao wanahimiza mabadiliko ya mifumo ya sheria zinazowakandamiza watoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga anataja sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kuwa ni kandamizi na imekuwa ikimkandamiza mtoto na kumnyima haki yake ya kupata elimu na hivyo kushindwa kutimiza ndoto zake.
Anahimiza jamii kutoa kipaumbele kwa mtoto wa kike kwa sababu wana uwezo wa kuendeleza vizazi vijavyo. Sanga, anasema ipo haja ya mabadiliko ya mifumo ya kisheria ambayo imekuwa kikwazo kwa mtoto wa kike.
“Ipo haja ya kuharakisha mchakato wa mabadiliko ya sheria kandamizi ikiwemo mila potofu ambazo zimekuwa zikididimiza maendeleo ya mtoto wa kike.
"Nina imani mtoto wa kike akipewa nafasi anaweza hivyo ni lazima jamii iendane na wakati sambamba na kuweka mazingira bora ya kumlinda mtoto," anasema Sanga.
Sanga anasema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokubali mikataba ya kimataifa kulinda haki za watoto. Mdahalo kuhusu kupinga ndoa za utotoni, ulioandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la C-Sema, unaibua wadau mbalimbali wanaopinga vitendo hivyo.
Katika mdahalo huo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba anakemea ndoa za utotoni. Anasema zimekuwa zikiwafanya watoto wa kike kukosa elimu na wakati mwingine kupoteza maisha wakati wa kujifungua.
“Inatakiwa tufike mahali sote tukubaliane kwamba ndoa za utotoni sasa basi ili kuwapa watoto wa kike fursa ya kupata elimu na baadae kuchagua wenza wanaowataka badala ya kuchaguliwa,” anasema.
Anasema watoto wengine wanaolewa na wanaume wasiowafahamu na hivyo kujikuta wakipata vidonda vya maisha moyoni kwa kuchaguliwa wenza. Mratibu wa C- Sema, Michael Kehongoh anasema kampeni ya kumtetea mtoto wa kike ni endelevu.
Anasisitiza kwamba, inahitajika sauti moja kuokoa watoto hao ambao wanategemea msaada na utetezi wa jamii kutimiza ndoto zao. Ndoa za utotoni nchini kwa kiasi kikubwa zinawakumba wasichana wenye elimu ndogo, wanaotoka katika familia masikini na wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Takwimu zinaonesha asilimia 61 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 20 na 24 ambao hawakusoma na asilimia 39 ya wenye elimu ya msingi waliolewa wakiwa na umri mdogo ikilinganishwa na wenye umri kama huo ambao wana elimu ya sekondari au zaidi.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Margareth Mussai anasema ndoa za utotoni ni sehemu ya unyanyasaji wa watoto wa kike.
Anakariri takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), kwamba katika kipindi cha miaka 10 ijayo wasichana wapatao milioni moja wanatarajiwa kuwa wameolewa katika umri wa chini ya miaka 18 dunini kote.
Anasema Afrika, asilimia 42 ya wasichana wote huolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18. Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa ndoa za utotoni, ukiwa na asilimia 59.
Mingine na asilimia kwenye mabano ni Tabora (58), Mara (55), Dodoma (51), Lindi (48), Mbeya (45), Morogoro (42), Singida (52), Rukwa (40), Ruvuma (39), Mwanza (37), Kagera (36), Mtwara (35), Manyara (34), Pwani (33), Tanga (29), Arusha (27), Kilimanjaro (27), Kigoma (29), Dar es Salaam (19) na Iringa (8).
Anasema katika kukabiliana na tatizo hilo, serikali inaendelea kuwaelimisha wazazi na walezi kutambua kwamba athari zinazotokana na uwepo wa ndoa za utotoni ni pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili.
Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, inahimizwa kuunga mkono jitihada za serikali katika kuwapatia watoto haki ya kusoma, kuishi na kuwalinda dhidi ya ndoa za utotoni. Kila mtu anapaswa kuwajibika na kuhakikisha kwamba mtoto wa kike haolewi katika umri mdogo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo