Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam limesema limefanikiwa kuudhibiti mtandao wa majambazi ambao baadhi yao walikuwa wameweka kambi katika moja ya misitu huko Vikindu Pwani, zikiwemo silaha za kijeshi ambazo zimekuwa zikitumika katika matukio ya kihalifu ikiwemo kuua askari watano wa jeshi hilo katika maeneo ya Mbande na Vikindu jijini Dar es Salaam.
Katika taarifa yake juu ya operesheni maalum ambayo jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam imeifanya mara baada ya kutokea kwa mauaji ya askari Polisi na uporaji wa silaha uliofanyika siku chache zilizopita kamanda wa polisi wa kanda hiyo Kamishna Simon Sirro amesema operesheni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani mpaka sasa wameweza kuudhibiti mtandao wa majambazi hao hatari ambao wamekuwa wakishirikiana na wenzao kutoka nje ya nchi kufanya uhalifu hapa nchini.
Kamanda Sirro amesema mafanikio hayo yamesaidiwa na taarifa walizotoa raia wema juu ya wahalifu hao na hivyo namewataka viongozi wa serikali za mitaa kufuatilia kila mtu anayeingia katika mitaa yao kwa kumfahamu vizuri ikiwemo shughuli anazofanya kwani wahalifu hao wamekuwa wakipanga nyumba Katika mitaa yao na kuzitumia kwa shughuli za kihalifu.
Mbali na hilo Kamanda Sirro amepiga marufuku uanzishwaji wa vikundi vya vijana na watoto kinyume na sheria ambao wamekuwa wakifundishwa mazoezi ya kijeshi na kuwaomba wazazi kuwa makini katika kuangalia mienendo ya watoto wao.
