Chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA Wilayani kahama mkoani Shinyanga kimeitaka serikali wilayani humo kurejesha mabati zaidi ya 800 yaliyotolewa na chama hicho kama msaada wa nyumba kwa waathirika wa mafuriko wilayani humo
Mwenyekiti wa CHADEMA Wilayani Kahama Juma Protas Ntaimpera amesema azimio hilo linatokana na msimamo wa serikali ya awamu ya tano kutokuwa na mpango wa kujenga tena nyumba hizo
Ntaimpera amesema mara baada ya serikali kurejesha mabati hayo chama hicho kitayagawa kwa watu wenye mahitaji ili wayatumie katika ujenzi kwa kuwa wananchi hao bado wanaoishi katika mazingira magumu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkulu amesema hana taarifa za msaada huo kutoka CHADEMA kwa kuwa wakati msaada huo ukitolewa hakuwa mkuu wa wilaya hiyo
Katika ziara yake wilayani Kahama hivi karibuni Rais John Magufuli alisema serikali yake haitatekeleza ujenzi huo ulioahidiwa na serikali ya awamu ya nne na badala yake kiasi cha shilingi bilioni 2 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo zitatumika katika miradi ya maendeleo
