Eneo la Matambiko lazua Gumzo Makete, Wazee watahadharisha

Imeelezwa kuwa kutokana na eneo la Ndacho lililopo kata ya Lupalilo wilayani Makete mkoani Njombe kuwa la kimila, na wananchi kuwekeza hapo na kufanya shughuli zao za kilimo pamoja na kutokuwepo kwa makubaliano mazuri ni miongoni mwa sababu zinazo kwamisha kuanza kwa ujenzi wa shule ya sekondari ya kata ya Lupalilo.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na wananchi wa kijiji cha Mago wakiwemo wamiliki wa eneo linalolalamikiwa juu ya ujenzi huo mbele ya mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya makete Bi Veronica Kesi ambaye ni afisa tarafa ya Lupalilo Bw Estomeki Kyando katika mkutano wa pamoja na wananchi hao, ambapo wamesema yapo madhara yatakayotokea endapo watakubali shule ijengwe hapo ikiwemo kuangamiza watoto watakaosoma hapo sababu ya eneo kuwa la kimila pamoja na rasilimali walizowekeza katika eneo hilo kupotea.
  
Wananchi waliojitambulisha kama wamiliki wa eneo hilo akiwemo Victon Sanga, na Aldo Lwango wamesema kuwa wao wanahitaji wajenge shule ya sekondari eneo lisilokuwa na mgogoro lililopo katika kijiji cha Mago na kuiomba jamii kuelewa kwamba wao hawapingi maendeleo ya kata kuwa na shule ya Sekondari bali wao wanapinga ujenzi kufanyika katika eneo la Ndatso

"Naomba niseme Ukweli, hapa mnaposema tujenge sekondari sisi hatukushirikishwa toka mwanzo, na huu mchakato naona kama umevunja sheria, hili eneo ni letu la kilimo, lakini tumewekeza mali zetu hapa, tumepanda miti leo imechomwa moto mingine imefyekwa, lakini hapa ni eneo la mila, kuna vichaka vile kule hakuna anayeingia kutokana na mila, lilikuja katapila kuchimba kifusi lilishindwa, mwenge wa uhuru ulizimika hapa, leo mnataka kujenga shule mnataka watoto wetu waje  wapate madhara? "amesema Bw. Aldo Lavango

Naye Mzee Peter Maekule ambaye ni miongoni mwa walioshiriki amesema tangu akiwa mdogo anatambua kuwa eneo hilo ni la mila na akasema kwa maoni yake anashauri shule ijengwe kwenye eneo jingine na si hilo kutokana na mpaka sasa baadhi ya wananchi wanalitumia kwa ajili ya mila zao

Aidha katika kikao hicho aliyekuwa diwani wa kata ya Lupalilo Mh. Manase Mwalukisa ambaye kwa sasa amestaafu na alikuwepo katika vikao vya awali vya ujenzi wa sekondari hadi alipostaafu amezungumzia mchakato ulivyokuwa tokea mwaka 2008 ambapo yeye alikuwa diwani kwa kusema wenye maeneo walishirikishwa na wakakubaliana shule hiyo ijengwe eneo la Ndatso

Amesema katika utawala wake vikao vilivyoketi kuhusu ujenzi wa shule hiyo wajumbe walikubaliana shule ijengwe katika eneo hilo na baada ya kupeleka mihutasari ya vikao wilayani wataalamu walifika na kukagua eneo hilo na kusema linafaa kwa ajili ya ujenzi wa sekondari hiyo na wenye maeneo hayo walishirikishwa

"Kiuhalisia hili eneo lipo katika kijiji cha Lupalilo na sio Mago, na wapo wamiliki kutoka kijiji cha Mago, Msema kweli ni mpenzi wa Mungu kama anavyosema rais wetu, mimi nakataa kuwa watu wenye maeneo haya hawakushirikishwa, si kweli wapo walioshiriki vikao na waliandika majina yao na walisaini na wasiojua kusoma na kuandika waliweka alama za dole gumba na kumbukumbu zipo" amesema Mwalukisa

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Mh. Imani Mahenge na Afisa tarafa Bw. Estomeki Kyando kwa pamoja wamesema kuwa kutokana na sababu zilizotolewa na wananchi wao watazipeleka kama zilivyo kwa Mkuu wa wilaya kwa hatua zaidi, na wakawasihi wananchi kupunguza jazba na badala yake jambo hilo waendenalo kwa umakini mkubwa ili wafikie mwisho mwema kwa kuwa kila mtu anapenda sekondari iwepo katika kata yao.

Mkuu wa wilaya ya Makete Mh Veronica Kesi amepanga ziaraya kufikaeneo hilo na kuzungumza na wananchi Septemba 15 mwaka huu kwa lengo la kutafuta muafaka ili ujenzi wa sekondari katika kata hiyo uanze kama mpang wa serikali unavyotaka kuwa kila kata iwe na shule ya sekondari
 Wananchi wakiwa kwenye Mkutano
 Mzee Peter akitahadharisha kuhusu eneo hilo la Mila na Matambiko

 Diwani Imani Mahenge

 Kichaka kilichopo katika eneo hilo lililotengwa kwa ujenzi wa sekondari kinachodaiwa ni eneo la mila
 Mwananchi akimuonesha mwandishi wetu eneo hilo ambalo hutumika kwa mila na matambiko



JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo