Zuio la shughuli za kisiasa lililowekwa na Jeshi la Polisi baada ya Rais John Magufuli kusema anataka kutekeleza ahadi zake za uchaguzi, limeibua mbinu mpya kwa wanasiasa na wananchi; sasa wanatumia mitandao ya kijamii kujadili siasa.
Jeshi la Polisi limekuwa likizuia mikutano na maandamano ya kisiasa kwa maelezo tofauti, ikiwa ni pamoja na kueleza kuwa ina viashiria vya kusababisha vurugu, inalenga kufanya wananchi wasitii mamlaka na wakati mwingine kutumia ugonjwa usiojulikana ulioua watu kadhaa mkoani Dodoma.
Lakini, tamko la Rais Magufuli kwamba uchaguzi umekwisha na hivyo wanasiasa wasubiri hadi mwaka 2020 kufanya kazi hiyo, ndiyo linaonekana kulisukuma jeshi hilo kuvibana vyama vya upinzani kuitisha mikutano na maandamano.
Wakati polisi ikizuia mikutano na maandamano, wanasiasa na wafuasi wao sasa wanatumia mitandao ya kijamii kuendesha siasa kwa kukosoa maamuzi ya Serikali na masuala mengine.
Mitandao ya kijamii hususan makundi ya WhatsApp, Twitter, Jamii Forums na Facebook kuna mijadala mikali inaendelea na kushirikisha watu wengi zaidi ya mikutano ya hadhara.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka (pichani) amesema wanaelewa kuwa kuna mwelekeo mpya wa baadhi ya viongozi wa upinzani kuhamishia siasa kwenye mitandao ya kijamii.
“Tumeona hiyo trend (mwelekeo) na sisi tutawajibu humo humo. Tuna vijana wazuri tu wanaoweza kujenga hoja zenye mashiko kwa Watanzania, tena zisizowagawa,” amesema ole Sendeka.
