Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) katika Halmashauri ya wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza, anashikiliwa na jeshi la Polisi wilayani Sengerema kwa tuhuma za kumpiga mwalimu mmoja wa shule ya msingi Mwabasabe, Shinane Nkonoki wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti vya taaluma kwa walimu wa shule za msingi na Sekondari wilayani humo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Naibu kamishna Ahmed Msangi amethibitisha kukamatwa kwa afisa huyo wa TAKUKURU aliyejulikana kwa jina la Edwin kwa tuhuma za kumpiga mwalimu huyo akiwa katika zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi ambapo amefunguliwa jalada la kesi katika kituo cha polisi Nyehunge wakati uchunguzi ukiendelea.
Katibu wa chama cha walimu Tanzania ( CWT ) wilaya ya Sengerema Ruhumbika Francis amesema CWT inatarajia kulifikisha suala hilo Mahakamani kufuatia kitendo cha afisa huyo kumdhalilisha mwanachama wake, huku mwalimu anayedai kupigwa shinane nkonoki akieleza chanzo cha tukio hilo.
Baadhi ya walimu walioshuhudia tukio hilo lililotokea Septemba 9 mwaka huu, majira ya saa tisa alasiri katika ofisi za mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Buchosa zilizopo Nyehunge, wameeleza kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na afisa huyo wa takukuru dhidi ya mwalimu Nkonoki.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Buchosa Chrispine Luanda hakuwa tayari kulizungumzia tukio hilo kwa undani.
