Mwili wa mtoto albino wafukuliwa kwa uchunguzi

MWILI wa mtoto mwenye albinism aliyefariki kwa maradhi hivi karibuni na kuzikwa Jumapili iliyopita, umefukuliwa chini ya ulinzi wa polisi ili ufanyiwe uchunguzi kutokana na kuibuka maneno yenye kutatanisha kuwa wakati akiugua alikuwa akivuja damu nyingi puani na kuvimba mwili.

Mtoto huyo, Michael Juma aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu, alizikwa pembeni mwa nyumba yao Alhamisi wiki hii katika kijiji cha Bunambiyu, wilayani hapa na kuwashangaza wakazi wa eneo hilo.

Katibu wa Chama cha Watu Wenye Albino Nchini (TAS), tawi la mkoa wa Shinyanga, Lazaro Anael alisema kitendo cha kuufukua mwili kimewashangaza na kwamba tangu taarifa za kifo cha mtoto huyo kujulikana, yamezuka maneno kuwa kifo hicho kina utata.

Alisema alishiriki mazishi, lakini kabla ya kufika nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo akiambatana na Mkurugenzi wa Shirika la Under the Same Sun, Vicky Mtetema, waliukagua mwili wa mtoto huyo na kubaini haukuwa na tatizo.

“Mimi nasema hivi maneno haya yanatoka wapi wakati mwili tuliukagua haukuwa na dosari yoyote wakati huo tulikuwa na Vicky Mtetema akiwa anaupiga mwili picha, viongozi wa kijiji na kata walikuwepo pamoja na majirani wakishuhudia kuwa salama na ndipo shughuli za maziko zilifanyika… sasa kitendo cha kufukua mwili hapo serikali inataka kuleta hofu,” alisema.

Diwani wa Kata ya Bunambiyu, Richard Sangisangi aliyekuwa amekataa mwili huo kufukuliwa na kugoma kuwaita majirani kwa ajili ya kufukua mwili ili ufanyiwe uchunguzi aliondoka na kusema kamwe hawezi kuchuma dhambi kwa kile alichokieleza walishuhudia mwili ukiwa salama na alifariki kwa mapenzi ya Mungu sio ushirikina au kukatwa mapanga kama ilivyozoeleka maeneo mengine.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jonathan Katela alisema kitendo cha kufukua mwili huo sawa na kurudisha majonzi kwa jamii na familia, lakini akasisitiza ameridhia kwa kuwa serikali imetaka mwili ufukuliwe kwa uchunguzi.

Kauli kama hiyo ilitolewa na baba wa marehemu, Juma Masudi aliyesema ametii amri ya serikali, lakini yeye binafsi hakuridhika kuufukua mwili wa mwanawe aliyedai aliugua maradhi ya kawaida na kupata matibabu kituo cha afya Bunambiyu.

Hata hivyo, baada ya mvutano, polisi walifanikiwa kufukua mwili huku Dk Hellen Kaunda aliyekuwepo eneo la tukio akiufanyia uchunguzi na kueleza haukuwa na dosari yoyote na kwamba alifariki kwa maradhi.

Msafara wa Polisi, Kitengo cha Upelelezi wilayani Kishapu kupitia msemaji wake kwenye eneo la tukio, Meshack Sumuni aliwaomba radhi wananchi na wazazi huku akiwatoa hofu kwa kitendo cha kufukua kaburi kuwa ni jambo la kawaida unapotoa utata.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo