Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
(DPP), amewagwaya wabunge watatu; Kangi Lugola wa Mwibara na wenzake
wawili, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya rushwa baada ya kuwafutia
mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu.
Licha ya Lugola, wabunge wengine ni Suleiman Ahmed Saddiq (Mvomero) na Victor Mwambalaswa (Lupa).
Wakati DPP akiwafutia mashtaka hayo na
kuwaachia huru, wabunge hao wamesema wanatafakari hatua za kuchukua
dhidi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kile
walichokiitwa kuwadhalilishwa kwa kuwafungulia kesi hiyo, waliyoiita ya
kisiasa.
Wabunge hao ambao wote wanatoka Chama
cha Mapinduzi (CCM), walikuwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC) walipandishwa kizimbani Machi 31.
Walikuwa wakikabiliwa na shtaka la
kuomba rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, Mbwana Magote.
Hata hivyo washtakiwa hao wote walikana
shtaka hilo huku Lugola baada ya kusomewa shtaka hilo na kesi
kuahirishwa akisema kuwa hiyo ni vita ya kisiasa ambayo haitawazuia
kuendelea kutumbua majipu.
Awali, kabl ya kesi hiyo kuitwa jana
mahakamani hapo, upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa upelelezi wa
kesi hiyo tayari umeshakamilika na ukaomba mahakama ipange tarehe ya
usikilizwaji wa awali.
Kufuatia taarifa na maombi hayo ya
upande wa mashtaka, mahakama hatua hiyo ya usikilizwaji wa awali
ufanyike jana, ambapo washtakiwa walitarajiwa kusomewa maelezo ya awali
ya kesi hiyo kabla ya kuendelea na ushahidi.
Hata hivyo baada ya kesi hiyo kuitwa
jana kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo hayo ya awali, Wakili wa
Serikali, Kishenyi Mutalemwa aliyekuwa akisaidiana na Wakili wa
Takukuru, Emmanuel Jacob, aliieleza mahakama kuwa DPP hana nia ya
kuenedelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Wakili Mutalemwa alisema kuwa DPP
ameamua kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao
chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai
(CPA).
Hakimu Respicius Mwijage aliyekuwa
akisikiliza kesi hiyo alikubaliana na maombi hayo ya DPP na kuamuru
washtakiwa hao waachiwe huru.
“Shauri hili linaondolewa kama DPP alivyoomba na washtakiwa mnaachiwa huru.”, alisema Hakimu Mwijage.
Akizungumza na waandishi wa habari baada
ya kuachiwa huru, kwa niaba ya wenzake, Lugola alisema kuwa tangu
walipofikishwa mahakamani hapo walianza na Mungu na wamemaliza na Mungu,
na kusisitiza kauli aliyoitoa siku walipandishwa kizimbani kuwa kesi
hiyo ni ya kisiasa.
“Kimsingi tangu mwanzo tulipofikishwa
mahakamani hapa moyoni mwetu tulianza na Mungu na tuliahidi kumaliza na
Mungu na tumemaliza na Mungu.”, alisema Lugola na kuongeza:
“Leo Mungu amejibu, tumeachiwa huru.
Tunawaambia Watanzania kwamba kesi tuliyofunguliwa ilikuwa ni ya kutunga
na ilitengenezwa kwa sababu za kisiasa.”
Lugola aliendelea kueleza kuwa kutokana
na uamuzi huo Serikali kupitia Takukuru hawakuwa na ushahidi dhidi yao
na kwama ndio maana wamebadilika hivyo kama kinyonga.
“Walisema kwamba wamekamilisha upelelezi na kuomba tarehe ya kutusomea maelezo ya awali, leo wanafuta kesi.”, alisema Lugola.
Alisema baada ya uamuzi huo sasa
wataendelea kuwatumia wananchi waliowachagua katika majimbo yao huku
wakiweka wazi kuwa wanakwenda kukaa na mawakili wao ili wajadili hatua
za kuchukua dhidi ya Takukuru.
“Tutakaa na mawakili wetu tutafakari ni
cha kufanya kutokana na udhalilishwaji huu tuliofanyiwa na baada ya hapo
ndio tutajua nini cha kufanya, lakini tunasikitishwa sana na
udhalilishwaji huu tuliofanyiwa na Takukuru.”, alisisitiza Lugola.
Akiwasomea washtakiwa hao shtataka hilo,
siku ya kwanza walipopandishwa kizimbani, Wakili wa Takukuru, Magela
Ndimbo alisema kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo, Machi 15, 2016,
kinyume cha kifungu cha 15 (2) cha Sheria ya Takukuru.
Alidai kuwa washtakiwa hao walitenda
kosa hilo wakiwa katika Hotel ya Golden Tulip, iliyoko eneo la Masaki,
wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam, na kwamba waliomba rushwa hiyo
ili waweze kutoa mapendekezo mazuri ya Taarifa ya Hesabu za halmashauri
hiyo za mwaka 2015/2016.
Hakimu Mkazi Thomas Simba anayesikiliza
kesi hiyo aliwaachia huru washtakiwa hao kwa dhamana kwa masharti ya
kuwa na mdhamini mmoja ambaye alisaini bondi ya Sh5 milioni na kutakiwa
kuwafikisa mahakamani hapo washtakiwa kwa tarehe na saa itakayopangwa.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa na hakimu
kutoka nje ya mahakama, washtakiwa hao wakingali bado kizimani,
walionesha kufurahia huku Saddiq na Lugola wakishangilia kwa kunyanyua
juu mikono yote miwili wakionesha ishara ya ushindi.
Sambamba na kushangilia huko, Lugola pia
aliwashukuru waandishi wa habari lakini akasema kuwa kesi hiyo ni virta
ya kisiasa tu ambayo haitawakatisha tamaa wale walio tayari kutumbua
majipu kuendelea kutumbua majipu hayo.
Nawashukru sana waandishi wa habari kwa
coverage yenu. Licha ya vita hii ya kisiasa lakini wale tulio tayari
kutumbua majipu tutaendelea kutumbua majipu.
